Jemah Makamba
KESI dhidi ya Salum Njwete ‘Scorpion’
anayedaiwa kumjeruhi kwa kumtoboa macho Saidi Mrisho, imeendelea kusikilizwa kwenye
Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri kutoa
ushahidi.
Shahidi namba mbili, Stara Sudi ambaye
ni mke wa mlalamikaji na shahidi namba tatu, Yahya Kisukari anayetajwa kuwa
mdogo wa Mrisho, walitoa ushaidi wao mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Flora
Haule wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Nasoro Katuga.
Wakili Katuga alianza na maswali kwa
shahidi namba mbili kabla ya kuhitimisha kwa shahidi namba tatu, huku Mahakama
hiyo ikishuhudia Wakili wa mshitakiwa akishindwa kumuuliza Stara maswali.
Wakili:
Shahidi unaishi wapi na unafanya kazi gani?
Shahidi 2: Naishi Mabibo Makuburi na ni
mama wa nyumbani.
Wakili:
Ulifunga lini ndoa na mume wako ambaye ni mlalamikaji?
Shahidi: Nilifunga ndoa na mlalamikaji
mwaka jana mwezi wa 10.
Wakili: Unakumbuka tarehe sita mwezi wa sita
mwaka huu nini kilitokea?
Shahidi: Nilikuwa nimelala usiku,
nikapigiwa simu na kusikia sauti ya mume wangu akiniambia yuko Buguruni na amechomwa
visu na ametobolewa macho, haoni.
Wakili: Uliwezaje kujua kuwa hiyo ni
sauti ya mumeo?
Shahidi: Niliweza kujua kutokana na
kuniita jina la Mama Hance na nikaitambua sauti yake, ambapo simu iliita tena
nikasikika mtu mwingine akisema twende Amana haraka.
Wakili: Baada ya hapo, ulichukua hatua
gani wewe kama mke?
Shahidi: Nilitoka mimi, mama yangu na
dada yangu tukaelekea Amana Hospitali.
Wakili: Ieleze Mahakama mlimkuta mgonjwa
katika hali gani?
Shahidi: Tulimkuta akiwa amewekwa
bandeji kwenye macho na pamba kwenye majereha ya mgongoni na tumboni.
Wakili: Je, uliweza kumhoji amefanya
nini majeraha hayo?
Shahidi: Niliweza kumuuliza, alinijibu
amechomwa visu na mtu ambaye hamjui, lakini aliweza kusikia watu wakimtaja kwa
jina la Salum na Scorpion.
Wakili: Baada ya hapo nini kiliendelea hospitali
ya Amana?
Shahidi: Mgonjwa alihamishwa kwenda
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa matibabu zaidi.
Wakili: Wewe kama mke, baada ya hapo na
kutajiwa jina la aliyemfanyia tukio, yeye alichukua hatua gani?
Shahidi: Nilikwenda Buguruni Kituo cha
Polisi na kutoa taarifa nikapewa askari wa kike, nikaenda naye Muhimbili ambako
alimhoji mgonjwa na baada ya kutajiwa jina la mtuhumiwa, akasema tuondoke
wakamkamate.
Wakili: Baada ya hapo nini kiliendelea?
Shahidi: Nilifika hospitali siku ya tatu
na kukuta madaktari ambao walisema mgonjwa wetu hawezi kuona.
Wakili: Uliishi na mume wako tangu mwaka
jana, uliwahi kusikia ana tuhuma zozote za wizi au kukamatwa na Polisi?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Je, hakuwa na kazi nyingine
zaidi ya kinyozi?
Shahidi: Hapana, hakuwa na kazi
nyingine.
Wakili wa Serikali alimaliza maswali na
kuiachia Mahakama kama ina lolote ambapo wakili wa utetezi, Juma Nassoro
alisema hana swali kwa shahidi huyo ambapo shahidi wa tatu alianza kutoa
ushahidi wake.
Wakili: Shahidi unafanya kazi gani?
Shahidi 3: Kinyozi saluni ya Rogerz,
Tabata Sanene.
Wakili: Hujawahi kusikia tuhuma zozote
za wizi kwa mlalamikaji?
Shahidi: Hapana sijawahi.
Wakili: Una muda gani hapa mjini?
Shahidi: Miaka minne.
Wakili: Mlalamikaji ni kaka yako kivipi?
Shahidi: Tumezaliwa na mama mmoja, baba
tofauti.
Katika kesi hiyo, wakili wa Scorpion
alimhoji maswali shahidi huyo namba mbili na sehemu ya mahojiano hayo ni kama
ifuatavyo:
Wakili: Unapafahamu Buguruni?
Shahidi: Sipafahamu.
Wakili: Kwa nini wewe na ndugu yako
mnakana kupafahamu Buguruni, mnaogopa nini?
Shahidi: Sipafahamu ila huwa napita tu.
Wakili: Wewe unajua Kiswahili vizuri? Kwa
nini unasema hupafahamu halafu unasema huwa unapita tu?
Shahidi: Sijawahi kushuka Buguruni.
Wakili: Hujawahi kwenda na kaka yako
Buguruni kununua simu?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Mara ya mwisho kuuza simu saluni
kwenu ilikuwa lini?
Shahidi: Hatujawahi kuuza.
Baada ya maswali hayo, wakili wa utetezi
alisema amemaliza maswali huku upande wa Wakili wa Serikali akiiomba Mahakama
iwapangie siku nyingine ya kuendelea na ushahidi.
Hakimu Flora aliahirisha kesi hiyo hadi
Januari 11 kuendelea na ushahidi huku mshitakiwa akirudishwa rumande.
0 comments:
Post a Comment