Mwandishi Wetu, Arusha
Joshua Nassari |
MBUNGE wa jimbo la Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari, amepongeza na kusifu jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu
ya Tano katika kuwaletea maendeleo wananchi wa maeneo mbalimbali nchini
wakiwemo wa jimbo lake.
Kufuatia hatua hiyo, Nassari ameahidi
kushirikiana bega kwa bega na Serikali ili kuhakikisha maendeleo yanakuwa
endelevu. Nassari ametoa pongezi hizo jana mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ambaye alikuwa katika majumuisho ya ziara yake ya siku kumi ya kikazi mkoani
Arusha.
Mbunge huyo ambaye alilazimika kuja
nchini kwa dharura akitokea masomoni nchini Uingereza ili kumuwahi Waziri Mkuu,
amesema ameridhishwa na hatua za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinazochukuliwa
na Serikali.
Amesema ziara ya Waziri Mkuu mkoani
Arusha, imesaidia kutibu majeraha na makovu makubwa yalitokana na matokeo ya
uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
"Kama kuna kiongozi ambaye hawezi
kuunga mkono jitihada hizi za kuwaletea maendeleo watu wetu, atakuwa na matatizo,”
amesema.
Ameongeza kuwa kitendo cha Waziri Mkuu
kuweka mikakati ya kushughulikia migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi ni
ushahidi tosha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwasaidia wananchi
wa kawaida.
Nassari amesema mwaka 1952 wazee wa Meru
walimtuma mtu kwenda Uingereza kuomba uhuru wa wananchi wa Arumeru ili waweze
kujitawala na kumiliki ardhi yao kutoka kwa wakoloni.
Amesema wazee hao walichukua uamuzi huo
baada ya kuchoshwa na vitendo vya unyanyasaji vilivyokuwa vinafanywa na wakoloni
dhidi yao. Lakini miaka 55 imepita tangu nchi ipate Uhuru bado migogoro na
mateso hayo yapo.
Hivyo amempongeza Waziri Mkuu kwa kuamua
kuitafutia ufumbuzi changamoto ya ardhi wilayani Arumeru jambo ambalo
litawawezesha wananchi kupata ardhi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za
kimaendeleo zikiwemo za kilimo na ufugaji.
Waziri Mkuu juzi alifanya ziara katika
wilaya ya Arumeru ambapo alisema Serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote
wa mashamba makubwa wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu
wamekiuka mkataba wa umiliki.
Alisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi atakuja mkoani Arusha kwa ajili
ya kufanya mapitio ya mashamba yote makubwa ambayo hayajaendelezwa na
kuyarudishwa Serikalini.
“Tufanya mapitio ya kila shamba ili
kujua linamilikiwa na nani na alipewa lini na tangu alipokabidhiwa amefanya
nini. Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu ameshindwa
kupata mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo,” amesema.
Amesema Serikali haiko tayari kuona
wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo kwa sababu ya watu wachache
kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza.
"Ninataarifa kwamba hapa Arumeru
kuna baadhi ya wawekezaji wanamiliki mashamba makubwa na hawajayaendeleza.
Wengine wanakodisha kwa wananchi ili kujipatia fedha kinyume na mikataba yao ya
umiliki. Hatutawavumilia,” alisema.
Alisema wilaya ya Arumeru inaongoza kwa
migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa na mtu mmoja mmoja na baadhi yao
wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kuwanyanyasa wananchi
wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo, ambapo aliwataka polisi kuacha tabia
hiyo mara moja.
0 comments:
Post a Comment