Mary Mtuka
Nembo ya Taifa |
SERIKALI imeahidi kumpa matibabu mmoja
kati ya wachoraji wa Ngao ya Taifa, Francis Ngosha na kumpa makazi ya kudumu.
Hatua hiyo imekuja baada ya kusambaa
picha kwenye mitandao ya kijamii zikimwonesha Ngosha akiwa na hali mbaya
Buguruni, Dar es Salaam, alikokutwa akiishi kwenye chumba kimoja alichopewa na
msamaria mwema.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye
hospitali ya Rufaa ya Amana, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalah alisema mchango wa mzee huyo ni mkubwa na
unathaminiwa na Serikali, hivyo ina jukumu la kuhakikisha anakuwa na afya bora.
"Kutokana na hali yake, tumeona kwanza
tushughulike na matibabu kwa sababu ndilo la muhimu na baada ya hapo tutamtafutia
makazi na kama atakubali atapelekwa katika kambi ya wazee wasiojiweza ya Nunge
au tumtafutie nyumba," alisema.
Alisema Mzee huyo alitumia kipaji chake
cha uchoraji jambo ambalo litadumu katika vizazi vyote vijavyo, hivyo Serikali
ilimwagiza kuchukua hatua za haraka za kumsaidia.
Mkuu wa Kitengo cha Dharura cha Hospitali
ya Taifa Muhimbili, Dk Juma Mfinanga alisema wamepokea taarifa hiyo kutoka kwa
Mkurugenzi Mkuu, ili kushughulikia kama ana tatizo la kiafya.
"Kwa mujibu wa wauguzi waliompokea
juzi na taarifa iliyopo ameonekana na uchovu hivyo ingawa tayari walishaanza
uchunguzi hivyo tutafanya uchunguzi zaidi ili kujua ni tatizo gani linamsumbua,"
alisema.
Mzee Ngosha alisema anaishi mwenyewe na mara
nyingi husaidiwa na majirani. Ngosha alizaliwa mwaka 1931 na hakubahatika
kupata watoto.
0 comments:
Post a Comment