Dotto Mwaibale
UTAFITI umeonesha kuwa wanawake ndio
waathirika wakubwa wa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa Tanzania Bara wakilinganishwa
na wanaume.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji
wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko wakati akitoa
taarifa jana kwa waandishi wa habari kwenye mkutano wa kujitambulisha kwao
tangu ateuliwe na Rais John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7.
Alisema maambukizi ya VVU kwa Tanzania
Bara ni asilimia 5.3 wanawake wakionesha kuathirika zaidi kwa asilimia 6.2 dhidi
ya wanaume ambao ni asilimia 3.8.
"Utafiti huo wa mwaka 2011 na 2012
ulionesha kuwa mkoa wa Njombe ulikuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ukiwa
na asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa asilimia 9.1 na Mbeya asilimia 9,"
alisema Dk Maboko.
Dk Maboko alisema Manyara ulikuwa na
kiwango kidogo cha maambukizi ya asilimia 1.5 lakini takwimu za ndani ya mkoa
huo eneo la Mirerani kwenye mgodi wa TanzaniteOne, maambukizi ya VVU yalikuwa
ni asilimia 16 kiwango ambacho ni cha juu ya mkoa wa Njombe.
Dk Maboko aliomba wananchi kokote waliko
kutobweteka kwa mafanikio ya mapambano dhidhi ya VVU na Ukimwi yawe endelevu
hata katika maeneo au mikoa ambako kuna maambukizi madogo ya VVU.
Alisema nchi inatakiwa kuweka nguvu
nyingi kifedha na kimkakati kwenye maeneo na makundi yenye kiwango kikubwa cha
maambukizi ya VVU ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti na ukusanyaji takwimu
za VVU na Ukimwi ili kuendelea kubaini na kupanga mipango dhidi ya ugonjwa huo
inayoongozwa na takwimu.
Aliongeza kuwa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloratibu mapambano dhidi ya Ukimwi (UNAIDS) limeweka malengo ya
muda wa kati ya tisini tatu (90-90-90).
90 ya kwanza inamaanisha asilimia tisini
ya watu wote wanaokisiwa kuwa na VVU kujua hali zao na 90 ya pili ikimaanisha
kuwa asilimia tisini ya waliobainika kuwa na VVU kuanza kutumia dawa za
kupunguza makali ya VVU (ARVs) mara moja na 90 ya tatu ya walioanza dawa waweze
kuwa na ufubazo endelevu wa virusi vya Ukimwi mwilini.
Dk Maboko alitoa mwito kwa wananchi, taasisi
za kijamii, Serikali, watu binafsi na kampuni za kibiashara kuchangia mfuko wa
udhamini wa masuala ya ukimwi (ATF) ulioanzishwa na Serikali ili kuondokana na
utegemezi kwa wafadhili.
0 comments:
Post a Comment