*Awashauri wapinzani kuhakikisha Katiba mpya inaandikwa
*Lowassa
akubali yaliyopita si ndwele sasa aganga yajayo
Celina
Mathew
Kingunge Ngombale-Mwiru |
MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru,
ameupa upinzani mbinu za kushinda uchaguzi mkuu mwaka 2020 na kwamba bila hivyo
wasahau kushika Dola huku akieleza kuwa mapambano kwa sasa ni makubwa.
Kingunge amewataka wapinzani kuhakikisha
wanazifanyia kazi changamoto hizo kabla ya uchaguzi ambazo ni kuwapo kwa tume
huru ya mabadiliko ya Katiba na sheria inayoruhusu matokeo ya uchaguzi wa rais
kuhojiwa mahakamani.
Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana alipokutana
na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuzungumza na vijana wanaojiita wapenda
mabadiliko, waliokamatwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana kutokana na makosa
mbalimbali na kusikiliza changamoto walizokutana nazo.
"Tunapopambana tuweke suala hilo
karibu, tufanye yote lakini tuhakikishe tunapata Katiba mpya au vipengee
vilivyo kwenye Katiba inayopendekezwa virekebishwe. Pia bila shinikizo kutoka
kwa wananchi, Serikali haitakubali kutuachia nchi, hivyo tambueni mapambano ni
makubwa, lakini tunayaweza," alisema.
Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa kama kuna
mtu anadhani anaweza kupata wema kwa kupewa na Mungu, shetani au miujiza
amepotea, kwa kuwa kila kitu ni matokeo ya mapambano.
Alisema yeye alianza kutafuta mabadiliko
siku nyingi akiwa sekondari na haikuwa rahisi kwake, kutokana na kuwa wengi
walikuwa wasaliti na hawakufanya kitu.
Alisema hatua ya yeye kuacha kazi na
kwenda kuitumikia TANU aligombana na baba yake, kwa kuwa hakupenda kitendo
hicho hata kusababisha baba yake amnunie kwa miezi sita.
"Napenda niwaambieni, mabadiliko
yanataka watu wenye moyo wa ujasiri, kwa maana mapambano ya sasa ni magumu
zaidi, kwa kuwa mazingira yamebadilika hivyo inahitajika nguvu kubwa ya vijana
kukabiliana nayo," alisema Kingunge.
Alisema, awali kulikuwa na utawala wa
Wakoloni na Waingereza licha ya kuwa wanyonyaji na wakandamizaji, walikuwa na
umoja wao, hawakupenda watu wajiunge na chama, lakini walikuwa wastaarabu.
"Jambo linaloshangaza ni kuwa
watawala wetu hawaheshimu sheria wala Katiba, mtatendewa mabaya sana, hivyo
muwe tayari kukabiliana nayo…hali ya sasa inahitaji vijana wenye moyo wa
mabadiliko," alisema na kuongeza:
"Chadema inakubalika na Lowassa
anakubalika, lakini katika mazingira ambayo kuna uongozi wa Serikali
usioheshimu Katiba, inabidi jitihada zifanyike na kubwa zaidi," alisema.
Lowassa
Lowassa alisema yaliyopita si ndwele na
kuwataka wapenda mabadiliko kuganga yajayo, kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2020.
Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati
Kuu ya Chadema, alitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa ujasiri na kuwashukuru kwa
kuchagua mabadiliko.
Alisema yaliyopita walikubaliana nayo na
kilichobaki sasa ni huhakikisha wanaunda jeshi kubwa, ili kuendelea na mjadala
wa kushinda ifikapo mwaka 2020.
Aliwataka vijana hao kuhakikisha kuwa hawakati
tamaa na kutumia changamoto walizopata kama mwanzo wa mafanikio.
"Tumejifunza kuhifadhi mafanikio
hayo, hivyo nawaomba msikate tamaa kwa maana naamini uchaguzi uliopita
tulishinda na unaokuja mwaka 2020 tutashinda tena kwa kishindo," alisema.
0 comments:
Post a Comment