Venance Nestory
Ridhiwani Kikwete |
MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema Sera ya
Elimu nchini inapaswa kuwaandaa vijana kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa Mahafali ya 15
ya Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam.
Alisema kuna ulazima wa kubadili mifumo ya elimu nchini
ili iweze kumkomboa kijana wa Kitanzania anayehitimu Chuo Kikuu badala ya
kumfanya mtumwa wa ajira.
“Mfano kwa siku ya leo pekee, vijana zaidi ya 550,
wametunukiwa Shahada za Umahiri na wengi wao hawana ajira ya kudumu, sasa kama
viongozi wa taifa hili tuna mikakati gani ya kuokoa vijana wanaohitimu kila
mwaka katika vyuo vyetu,” alihoji Ridhiwani.
Ridhiwani aliendelea “Ukiachana na hilo tuna dhana potofu
miongoni mwetu hasa kutowapa nafasi mbalimbali vijana waliohitimu vyuo mbalimbali
kwa kigezo cha kukosa uzoefu. Nawaombeni waajiri tuwape nafasi hawa vijana
wajifunze na kuonesha uwezo wao.”
Ridhiwani alisema ni vyema hatua za haraka zikachukuliwa dhidi
ya wahitimu kwa kuwapa mitaji ili kutatua janga la vijana wasio na ajira katika
jamii inayotuzunguka.
Alisema suala hilo linapaswa kuwa na jamii nzima, ikiwamo
taasisi za kifedha ambazo nazo zinapaswa kuwaamini vijana hao na kuwapa mikopo
yenye riba nafuu kwa ajili ya kuanzisha biashara.
“Nimebaini kuna vijana wenye uwezo mkubwa wa kufanya
tafiti na wanatambua umuhimu wa mafanikio katika elimu zao ila hawana mitaji na
wanahitaji kusaidiwa kifedha na vitendea kazi,” alisema.
Iwapo mazingira bora ya kujiajili yataandaliwa kwa vijana
tutapunguza wimbi la vijana wasio na ajira mitaani na kuendana na Sera ya Serikali
iliyopo madarakani ya kukuza uchumi wa viwanda.
0 comments:
Post a Comment