Mpoki Bukuku |
MPIGAPICHA mwandamizi wa
kampuni ya The Guardian Limited, Mpoki Bukuku (44), amefariki dunia.
Bukuku alikumbwa na mauti
jana asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu
baada ya kupata ajali juzi usiku Mwenge, Dar es Salaam.
Taarifa za ajali ya Bukuku
zilianza kusambaa jana asubuhi, zikieleza kuwa alivunjika miguu na mkono wa
kushoto katika ajali hiyo ya kugongwa na gari akitembea kwa miguu na
kiukimbizwa Muhimbili.
Akizungumza na
gazeti hili jana kwa simu, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Taasisi ya
Tiba ya Mifupa ya Fahamu (MoI), Almas Jumaa, alisema Bukuku aliaga dunia saa nne asubuhi jana wakati madaktari wakimhudumia.
“Tulimpokea Bukuku
kutoka MNH, leo (jana) saa 11 alfajiri baada ya kupata ajali ya gari
iliyosababisha kuumia akivunjika baadhi ya viungo vyake,” alisema.
Alisema wakati
wanampokea, majeruhi alionekana na maumivu upande wa kushoto wa mwili na
madaktari walibaini ndiko alikoangukia.
Almasi alisema
Bukuku alivunjika mbavu tatu za kushoto, miguu na mkono wa kushoto.
“Alikuwa na
michubuko mwilini hasa kichwani, lakini alionekana na majeraha kwa ndani ya
mwili,” alisema Almas.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Guardian Limited, Richard Mgamba katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, alielezea namna alivyopokea taarifa za msiba huo.
“Kama ilivyo kwa wengine
wengi, nilipokea kwa mshituko mkubwa na kutoamini kifo cha ghafla cha mmoja wa
wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Mpoki Bukuku, aliyefariki dunia
Muhimbili.
“Kwa familia yake, wamepoteza
baba, mume na zaidi ya yote rafiki wa kweli, lakini kwetu sisi The Guardian
Limited, tumepoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa
habari,” alisema Mgamba.
Mgamba alisema Bukuku alikuwa
mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote, lakini katika uandishi wa habari, aliipenda
fani yake na hakuogopa kupambana ilimradi apate habari nzuri.
Alifafanua kuwa ujasiri wa Bukuku
uliosababishwa na kiu yake ya kupata habari nzuri kuliko wengine, wakati
mwingine ilimweka matatani.
Kupigwa
“Wale wanaoelewa uandishi
wa habari wa picha, watabaini kwamba ujasiri na kuipenda kazi ni sifa kuu mbili
za kila mpigapicha, ili apate habari nzuri na yenye nguvu. Bukuku alikuwa na
sifa zote hizo. Alikuwa shujaa na mwenye mapenzi na kazi yake, hasa wakati
akifuatilia habari kubwa kokote nchini.
“Alipigwa na hata kuteswa
na maadui wa uhuru wa vyombo vya habari, lakini bado mahaba yake katika
kufanikisha habari bora hayakuzimwa. Alikuwa mwandishi wa habari si kwa bahati
mbaya, bali kwa kuchagua na ndiyo maana alikuwa na mapenzi wakati akitimiza
wajibu wake wa kutekeleza kazi za kihabari alizopangiwa na wahariri wake,”
alisema na kuongeza:
“Bukuku amemaliza safari
yake duniani, kimwili hayuko nasi lakini kiroho na kiweledi, mara zote atakuwa
nasi daima. Sisi katika The Guardian Limited tunaungana na familia, ndugu na
marafiki katika kipindi hiki kigumu, kuomboleza msiba wa mtu ambaye tumekuwa
tukifanya naye kazi kwa miaka mingi.”
Mgamba aliongeza kuwa kampuni
hiyo itaunga mkono kwa ukamilifu familia ya marehemu Bukuku, ambapo kwa niaba
ya wafanyakazi wa The Guardian Limited, alitoa salamu za rambirambi kwa
mjane wa Bukuku, Lucy, watoto na wadau wote wa tasnia ya habari nchini, kwa
kifo cha ghafla na cha kushitua cha mmoja weo.
Waziri
Waziri wa
Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alituma salamu za rambirambi kwa
familia, ndugu, jamaa wapiga picha pamoja na wanahabari wote nchini, kwa kifo
cha Bukuku.
Taarifa ya Wizara
ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari,
ilieleza kuwa Nape pamoja na watendaji wa Wizara walipokea kwa masikitiko makubwa
taarifa za kifo cha mwanahabari huyo, kwani ni pigo kwa tasnia ya habari nchini.
“Nimepokea kwa
masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mwanahabari Mpoki Bukuku. Kifo chake ni
pigo kwa tasnia ya habari hususan katika picha , nimehuzunishwa sana kwa sababu
marehemu wakati wa uhai wake, alitoa mchango mkubwa kwenye vyombo vya habari yakiwamo
magazeti ya Majira, Business Times , The Guardian , Nipashe, Mwananchi na The
Citizen,” alisema Nape katika taarifa hiyo na
kuongeza:
“Mungu ailaze
roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amina.”
0 comments:
Post a Comment