Majaliwa agundua ‘janja ya nyani’


Seif Mangwangi, Singida

Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kwa mara ya kwanza amegundua ujanja wa wafanyabiashara wanaoingiza mafuta ya kula nchini kukwepa kodi ya Serikali kwa kuweka kimiminika cha kutengenezea sabuni kwenye mafuta masafi ili yaonekane kuwa ni machafu.

Kufuatia hali hiyo, Majaliwa amesema atapambana na wafanyabiashara hao ili kuokoa mamilioni ya msamaha wa pesa za kodi ambayo walikuwa wakipewa kwa madai ya kuingiza nchini mafuta machafu.

Akizungumza juzi baada ya kutembelea kiwanda kikubwa Afrika cha kukamua na kusindika mafuta ya kula ya alizeti cha Mount Meru Millers, Waziri Mkuu alisema ziara yake katika kiwanda hicho amegundua jambo hilo ambalo ni hatari kwa uchumi wa nchi.

“Sasa nimegundua ujanja ambao wafanyabiashara hawa wanaoufanya, wamekuwa wakiagiza kontena za mafuta ya kula na kuweka kimiminika ambacho hutumika kutengenezea sabuni, ili yakipimwa yaonekane kuwa ni mafuta machafu, hata hivyo mafuta wanayoingiza yana kiwango kikubwa cha lehemu ambayo si nzuri kwa afya,” alisema.

Alisema anashangazwa pia na watendaji wa bandari ya Dar es Salaam yanakopitia mafuta hayo, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kushindwa kubaini ujanja huo ambao umekuwa ukiikosesha Serikali mamilioni ya kodi na kukandamiza wafanyabiashara wa ndani.

Majaliwa alisema lengo la Serikali ni kuinua viwanda vya ndani na kuongeza mapato ya wakulima nchini, lakini lengo hilo limekuwa likikwamishwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao hutumia mbinu za hali ya juu kukwepa kodi.

“Kwa kweli hii mbinu wanayotumia hawa wafanyabiashara ni ya hali ya juu kabisa, nitahakikisha napambana nao kwa kuwa hili suala la kuingiza mafuta machafu limekuwa likitusumbua sana, huu msamaha wa kodi sasa utafutwa,” alisema.

Waziri Mkuu alimtaka mwekezaji huyo, kupanua wigo wa kununua alizeti kwa wakulima wa Kanda ya Kati, ikiwamo kuongeza bei ya ununuzi na kwamba Serikali itahakikisha inamtengenezea mazingira mazuri ya biashara hiyo.

“Sasa kwa kuwa nimegundua haka kamchezo tunakofanyiwa na hawa wafanyabiashara, nikuhakikishie kuwa tuko bega kwa bega  na wewe kuhakikisha kilimo cha alizeti kinakua maradufu ili kunyanyua wakulima wetu, na wewe ongeza bei ya ununuzi, tutakusaidia pale unapokwama,” alisema.

Akijibu kauli hiyo ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho, Atul Mittal alitangaza bei mpya ya kununua alizeti kutoka Sh 850 hadi 1,000 kwa mbegu bora na safi aina ya Serena na bei ya Sh 800 hadi Sh 870 kwa aina zingine za alizeti.
                                                                                                   
Waziri Mkuu alipongeza bei mpya aliyoitangaza mwekezaji huyo mzawa na kuwataka wakulima kupeleka alizeti zao kiwandani hapo ili kuweza kupata faida kwa mazao waliyolima na kuhamasika kulima zaidi msimu ujao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo