*Nchi zasaini mikataba mitatu ya maendeleo
*Kushirikiana
kwenye umeme, usafiri wa anga
Celina Mathew
Hailemariamu na Rais Magufuli |
RAIS John
Magufuli na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn wamekubaliana mambo
15 likiwemo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya nishati ya umeme nchini.
Baadhi ya maeneo
waliyokubaliana ni utalii, viza, kilimo, kufundisha mashirika ya mawasiliano,
elimu, mifumo ya kodi, kufungua ubalozi Dodoma, viwanda, madini, ushirikiano
katika majeshi, matumizi ya Mto Nile, ujenzi wa bwawa la umeme na ushirikiano
kwenye mashirika ya ndege ya nchi hizo mbili.
Akizungumza Dar
es Salaam jana baada ya kukubaliana masuala hayo, Rais Magufuli alimwomba
Waziri Mkuu huyo kutuma wataalamu wa masuala ya umeme ambao wamejenga bwawa la
Gibe linalozalisha umeme wa megawati 1,870 nchini humo kuja nchini.
“Kwa kuwa Waziri
Mkuu Desalegn ameniambia Ethiopia ina wataalamu wa kuzalisha umeme wa bei nafuu
na wana mpango wa kujenga bwawa kubwa zaidi la kuzalisha umeme wa megawati
6,000 nimemwomba alete wataalamu wake hapa ambao nitawaonesha eneo ili waweze
kutuzalishia umeme,” alisema.
Alisema nchi
ikitaka kujenga uchumi wa viwanda lazima uwepo umeme wa uhakika hivyo
atahakikisha anatumia fursa hiyo, kwa kupeleka wataalamu hao kwenye maeneo ya Mto
Rufiji ili waweze kuzalisha umeme wa kutosha.
Alisema Waziri Mkuu
Desalegn aliahidi kuwa ataiongeza Tanzania megawati 400 kutoka kwenye bwawa
lake, kwa kuwa huwa zinatumika hadi mpakani na Kenya, hivyo zitafika hadi
Tanzania.
“Pia tumejifunza
kuwa bei zao za umeme ziko chini ambapo megawati moja ni senti sita hadi saba,
nikafikiria kwa nini asituongeze nasi kwa kuwa italipa fursa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kujifunza kuwa kuna watu wanaozalisha umeme wa bei ya chini
kuliko kuuza bei ya juu kama ilivyo sasa,” alisema.
Akifafanua, Rais
Magufuli alisema kwenye suala la elimu, Waziri Mkuu huyo alimhakikishia kuwa
atachagua chuo kimoja nchini humo kwa ajili ya kufundisha somo la Kiswahili na
aliahidi kumpa wasomi na walimu wa kwenda kufundisha somo hilo Ethiopia.
Kuhusu matumizi
ya Mto Nile alisema wamekubaliana yanufaishe nchi zote zilizo kando ya Mto huo na
usiwe wa nchi moja.
Aliongeza kuwa
serikali ya Ethiopia imekubali kutoa ushirikiano mkubwa kwa Shirika la Ndege la
Tanzania (ATCL) kwenye masuala ya kibiashara.
Alisema kutakuwa
na eneo kubwa la kuhifadhi mizigo ambayo itakuwa ikisafirishwa kupitia nchini
kwenda Ethiopia na kwamba shirika lao hivi sasa lina ndege zaidi ya 96 na
wameagiza mpya 42 na wana maeneo ambayo ndege zao zinakwenda zaidi ya 92 huku
maeneo ya kawaida yakiwa 20 duniani.
Rais Magufuli
aliongeza kuwa Ethiopia itatumia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhifadhi mizigo
itakayosafirishwa na ndege zao.
Aidha, licha ya
kuwa Tanzania ina mifugo mingi bado haijainufaisha nchi kwa kuwa Ethiopia ina
viwanda vya ngozi, nyama na maziwa hivyo mifugo ni mingi na inawanufaisha
tofauti na nchini.
Aliongeza kuwa
kuna changamoto ya utoaji viza ambayo imekuwa ikikwamisha biashara kati ya nchi
hizo ambapo aliahidi kuhakikisha zinaondolewa.
Waziri Mkuu Desalegn
alisisitiza suala la kilimo na kueleza kuwa maendeleo kwa sasa yanaelekea
Afrika baada ya kutoka Ulaya na Marekani endapo suala hilo litapewa kipaumbele.
Alisema wakulima
wa Tanzania na Ethiopia wakishirikiana, wataleta mapinduzi makubwa kwenye
kilimo na kuwa endapo dola milioni za Marekani 100 zitatolewa kwa kila familia,
hususan kwa wakulima wadogo, nchi hizo zinaweza kuzalisha fedha nyingi.
“Viwanda
vijengwe wakati tukijitahidi kutumia teknolojia kubwa ya kisasa ili kufika
mbali, pia tunaweza kutumia idadi ya watu chini ya miaka 35 kuleta mabadiliko
kwa nchi hizi mbili na kuwaondoa kwenye umasikini,” alisema Waziri Mkuu.
Mikataba
Mikataba iliyosainiwa
kati ya Ethiopia na Tanzania ni pamoja na wa mkakati wa ushirikiano kati ya nchi
hizo, ambao unalenga kupambana na
wahamiaji haramu; ushirikiano kwenye mambo ya biashara na uwekezaji; masuala ya
afya, hususan katika kupambana na malaria na ushirikiano katika masuala ya
teknolojia.
Mkataba mwingine
ni wa kuanzisha Kamisheni ya Pamoja ya Kudumu ya nchi hizo, ambao unalenga
kuanzisha Tume ya Kudumu kati ya Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo kwa
kushirikiana na sekta zingine katika ushirikiano kwenye masuala ya kijamii na
uchumi.
Mwingine ni wa hati
ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya utalii. Kwa mujibu wa Rais
Magufuli, makubaliano hayo yanatoa fursa za uwekezaji na mafunzo kwa wadau wa
sekta ya utalii.
0 comments:
Post a Comment