Kamishna Robert Boaz |
WAKATI Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu
Nchemba akidai maiti saba iliyopatikana eneo la Mto Ruvu ni wahamiaji haramu,
Jeshi la Polisi limesema halijawafahamu watu hao kwa kuwa linaendelea na upelelezi.
Aidha, limesema linaendelea na upelelezi
kuhusu taarifa za kupotea kwa Bernard Focus ‘Saaanane’ ambaye ni mtumishi ndani
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyetoweka Desemba 5 mwaka huu.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kamishna Robert Boaz, alisema Desemba
9 mwaka huu miili hiyo ilikutwa mto Ruvu eneo la Makurunge wilaya ya Bagamoyo.
“Baada ya taarifa hizo kupatikana
zilifikishwa kituo cha polisi ambapo polisi na madaktari walifika eneo la tukio
na kufanya uchunguzi wa kitaalamu,” alisema.
Alisema miili sita ilionekana kuwa na
hali mbaya hivyo waliamua kuizika eneo la tukio, huku maiti moja ikichukuliwa
na kupelekwa hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kuhifadhiwa na kufanyiwa uchunguzi
na utambuzi zaidi.
Alifafanua kuwa hadi Desemba 16 maiti
hiyo haikutambulika na ndipo Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuamua kuizika.
“Kumekuwepo na taarifa nyingi kwenye
vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kudai maiti kuzikwa mapema, huku tukio
likiwa halipewi uzito unaostahili,” alisema.
Alisema kuwa wananchi wanapaswa kujua
kuwa hatua za kitaalamu zilifuatwa huku wakiendelea kufanya upelelezi unaolenga
kuwatambua marehemu pamoja na kujua kilichowasibu.
Wakati huo huo, Kamishna Boaz alisema
jeshi linachunguza taarifa ya kupotea kwa kwa mwananchi Focus ‘Saanane’ ambapo
jalada la uchunguzi limeshafunguliwa.
“Tunashukuru wananchi ambao wamekuwa
pamoja nasi wakitupatia taarifa mbalimbali na tuahidi kwamba taarifa hizo
tunazifanyia kazi,” alisema.
Akijibu swali juu ya uwepo wa Saanane
katika maiti saba zilizopatikana mto Ruvu, Kamishna Boaz alisema “Sina jibu
sahihi kwamba ndiye au siye.”
Kamishna Boaz aliwataka wananchi kuwa
watulivu wakati jeshi la polisi linapoendelea na upelelezi kuhusu t ukio hilo.
0 comments:
Post a Comment