Abraham Ntambara
WAKATI Serikali ikizitaka Taasisi zenye
leseni za mawasiliano nchini zikiwamo kampuni za simu kuhakikisha zinawekeza
asilimia 25 ya hisa zao kwa Watanzania kabla ya keshokutwa kwa kuzingatia
sheria ya soko la hisa na dhamana, wakazi wa Dar es Salaam wamesema hawana
uelewa mzuri wa masuala ya hisa.
Hivyo wameiomba Serikali kuendesha
kampeni maalumu ya kuwaelimisha juu ya suala hilo na namna watakavyozinunua.
Wakizungumza na JAMBO LEO jana kwa
nyakati tofauti, baadhi ya wakazi hao walisema Serikali ina nia njema kwa
wananchi wake lakini inatakiwa elimu ya ufahamu wa hisa.
Ally Said alisema kuna uelewa mdogo
miongoni mwa wananchi juu ya suala la hisa akieleza kuwa mtu anapoelezwa kitu
cha namna hiyo ni vigumu kuelewa.
“Serikali ina nia nzuri, lakini
inatakiwa kazi ya zaida katika kuelimisha wananchi,” alisema Said.
Philemon Mfugalo alibainisha kwamba
kunahitajika semina zitakazoelezea kwa undani kuhusu hisa ili kuamsha wananchi
na kujua jinsi watakavyopata asilimia hizo kwa kuzinunua na kujua watakavyonufaika.
Aidha, aliongeza kuwa kutokana na uelewa
mdogo, baadhi ya wananchi watashindwa kununua hisa hizo kwa kuhofia kuwa
wanaweza kuibiwa.
“Suala hili ni zuri kiuchumi kwa
mwananchi, ila inatakiwa wataalamu wa masuala ya uchumi kwa kushirikiana na Serikali
wafanye kampeni maalumu kuufahamisha umma juu ya hilo,” alisema Mfugalo.
Hawa Rajabu alisema hana taarifa za Serikali
kuzitaka kampuni za mawasiliano kuuza asilimia 25 ya hisa kwa wananchi na
kubainisha kuwa zilikuwa ngeni kwake.
Pia alieleza kutolewa chochote kuhusu
hisa akisema kutokana na hali hiyo hawezi kuzungumza lolote kuhusu hisa.
“Sina uelewa wowote, kwa hiyo siwezi
kuongea lolote kuhusu hisa,” alisema Rajabu.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari
Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa alizitaka kampuni zote ambazo leseni zao zilitolewa kabla ya Julai mosi
kuuza hisa hizo kwa wananchi na kujisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam
(DSE) kwa kipindi kisichozidi miezi sita tangu kuanza kwa kipindi hicho.
0 comments:
Post a Comment