Waandishi Wetu
WAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM)
kikifanya mabadiliko ya mfumo wake wa uongozi, ikiwa ni pamoja na kuondoa baadhi ya nafasi na kupunguza
idadi ya vikao, vyama vya upinzani nchini vimesema hayawezi kuwayumbisha wala
kukwamisha harakati zao za kutaka kushika dola.
Huku wakijigamba kuwa wamekuwa wakiibuka
na ushindi katika chaguzi mbalimbali lakini ushindi huo unaporwa na CCM, walisema
pamoja na mabadiliko hayo, chama hicho tawala ni kile kile kilichobadilika ni
muundo tu.
Hivi karibuni chama hicho kilifanya
mabadiliko yanayolenga kubana matumizi na kuongeza ufanisi, huku baadhi ya watu
wakipitiwa na panga hilo la mabadiliko, wakiwemo makatibu wasaidizi wa mikoa 32
na wilaya 139 sambamba na kupunguzwa kwa wajumbe 230 wa Halmashauri Kuu kutoka
288 hadi 158, wajumbe 10 wa Kamati Kuu kutoka 34 hadi 24.
Fagio hilo pia limewaondoa wajumbe
watatu wa kamati ya siasa ya mkoa, huku ikipunguza wajumbe wanne katika Kamati
ya Siasa ya Wilaya sambamba na kufyeka vyeo ambavyo havijatamkwa kwenye Katiba
ya chama hicho.
Mtazamo wa wapinzani
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika alisema, “CCM ni ile ile na uongozi
wake ni uleule. Mabadiliko hayo madogo waliyoyafanya hayawezi kuzuia haja na
hoja za mabadiliko.”
Mbunge huyo wa Kibamba alisema wananchi
wanahitaji mabadiliko makubwa kupitia Ukawa, huku akibainisha kuwa kama CCM
ingekuwa imejipanga, Rais John Magufuli angeruhusu kufanyika kwa mikutano ya
hadhara, kama ilivyokuwa awali.
“Ukawa tunachopaswa kufanya sasa ni kuwaongoza
wananchi kudai Tume huru ya uchaguzi ili iwe rahisi kuwashinda CCM mwaka 2020,”
alisema Mnyika na kuongeza;
“Kwa sasa tumewabaini mbinu na hujuma
zao kwa hiyo tumejipanga mapema. Kupitia mikutano hii ya ndani waliyoiruhusu,
tutajipanga kupambana nao.”
Katibu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Juju
Danda alisema mabadiliko ya CCM hayawezi kuwa na tija katika vyama vya upinzani
iwapo Katiba haitakuwa inafuatwa.
Alisema kwa muda mrefu kumekuwepo
maamuzi ya mtu mmoja katika kila jambo, hivyo hata kama wangekuwa wana CCM
wawili wanaweza kuwa kero au raha kwa wapinzani iwapo watafuata Katiba.
“Hapa hatuzungumzii mabadiliko yao kuwa
ya wengi au wachache, ila tunataka Katiba ifuatwe na kila mmoja wetu kwa sababu
ndio inatuongoza, si mtu kuamua hakuna mikutano halafu afuatwe,” alisema.
Alisema kitendo cha mwenyekiti wa CCM,
John Magufuli kupunguza idadi ya wajumbe si kwamba anakipenda chama au Serikali
ila msingi wake ni kujitawalisha madaraka na kusababisha wanachama wamuogope.
Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK),
Constatine Akitanda alisema mabadiliko ya CCM hayawezi kuleta mabadiliko, huku
akisisitiza kuwa usawa utapatikana iwapo kutakuwa na uwanja huru wa kufanya
siasa.
“Siasa sawa inategemeana na ngoma ambayo
itapigwa ambapo ni uwanja sawa. Sasa kwa hapa nchini hakuna uwanja sawa hivyo
ni ngumu kusema kuna fursa kwetu,” alisema.
Alisema CCM na Serikali wanapaswa
kutambua kuwa siasa ni maisha ya watu hivyo inapaswa kuheshimu na kutoa
ushirikiano baina yetu.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma
(Chauma), alisema haamini katika mabadiliko hayo na kuwataka wateule kusimamia
misingi ya haki na kuwa wavumilivu, kwani siasa ni mchezo wa uvumilivu zaidi.
Rungwe alisema CCM imekuwa katika wakati
mgumu kwa kipindi cha hivi karibuni, ila kupitia mabadiliko hayo inaweza kupotea
zaidi na kuwa wanachopoteza kwa sasa ni kufanya ubadhirifu katika halmashauri.
“Kimsingi sisi tunafanya kazi kwa mujibu
wa Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5, lakini kikwazo kikubwa ni kutofuatwa kwa
Katiba,” alisema.
Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alisema
kiujumla wateule wapya si tishio kwa siasa za Tanzania, ila alitoa angalizo kwa
kutaka wapewe muda zaidi ili waweze kupimwa.
“Tuwape muda hawa ndio wapiya pamoja na
ukweli kuwa si watu wa kutisha,” alisema.
Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashi Mohamed
alisema mabadiliko hayo ya CCM ni ya kupongezwa na kuwa vyama vya upinzani
vinapaswa kuiga njia hiyo.
Alisema hakuna haja ya kuangalia
mabadiliko hayo kwa misingi ya kukabiliana na wapinzani ila ni vema vyama vya
upinzani na viongozi wake kujifunza zaidi njia ya kufanya kazi kwa kujitathmini
zaidi.
0 comments:
Post a Comment