Suleiman Msuya
MGOGORO wa baadhi ya wakazi wa kijiji
cha Epanko kilichoko Kata ya Nawenge wilayani Ulanga na mwekezaji wa kampuni ya
TanzGraphite (TZ) Limited, unaelekea ukingoni, baada ya kampuni hiyo kueleza
kuwa inajipanga kulipa fidia kwa wakazi 388 watakaoathirika na uwekezaji huo
ifikapo mwakani.
Msemaji wa kampuni hiyo, Nassor Said, alitaja
mali zitakazolipwa fidia kuwa ni pamoja na nyumba, mashamba na makaburi.
Alisema pamoja na kulipa fidia hiyo
kampuni pia itatekeleza madai mengine kadhaa ya wananchi hao, ikiwamo ujenzi wa
kiwanja cha mpira, zahanati na wazee kukatiwa bima ya afya jambo ambalo pia
wamekubali kutekeleza.
“Ninachokiona hapa ni wananchi wa Epanko
wanahitaji elimu zaidi hasa kundi la wachache ambao kila kikucha wanaibuka na
kulalamika,” alisema.
Said alibainisha kuwa hakuna uchimbaji
ambao utaanza bila hatua zote muhimu kukamilika, hivyo hakuna sababu ya
wananchi kuwa na hofu na mradi huo.
Mgogoro
Hivi karibuni wakazi wa kijiji cha Epanko,
walijitokeza na kubainisha kuwa wamekuwa wakipatiwa vitisho kutoka kwa
mwekezaji huyo na Serikali, hali ambayo imewafanya waishi kwa hofu.
“Ni takribani mwaka mmoja tunaishi kwa
shida sana kwani sisi unatuona hapa tunashindwa kurejea kijiji kwetu kwa kuhofia
kukamatwa, kwani wenzetu wawili wamekamatwa na polisi kutokana na agizo la Mkuu
wa Mkoa Dk. Kebwe Steven,” alisema mmoja wa wakazi hao.
Alieleza kuwa mgogoro uliopo unatokana
na mwekezaji huyo kushindwa kufuata taratibu za uwekezaji kama Sheria ya Madini
ya 2010.
Diwani
Akizungumzia sakata hilo Diwani wa Kata
ya Newenge ambapo kijiji hicho kipo Protas Lukombe, alisema mgogoro huo
ulikuwepo ila kwa sasa umeanza kutatuliwa.
Diwani huyo alisema mwanzoni alikuwa na
kundi hilo ambalo linatetea maslahi ya wananchi na kuandika barua kwenda kwa
waziri mkuu, ila baada ya kupata elimu kuhusu suala hilo yupo tayari kuhama na
kuachia wawekezaji hao.
Mwenyekiti
CCM
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Wilaya ya Ulanga, Khalid Naloto alisema mgogoro huo upo kwa muda na anaufahamu,
lakini anavyojua, kuna juhudi zinafanyika kutatua.
Alisema kamati ya siasa ya wilaya
inatarajia kufanya ziara Desemba 21 na 22 katika kijiji cha Epanko ili kuweza
kupata muafaka wa suala hilo kwa wakati na wananchi kuendelea na shughuli zao.
“Naomba unipe nafasi nalifanyia kazi
sualah ilo kwani ni suala ambalo linahitaji kupata taarifa kamili,” alisema.
RPC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Ulrich Matei, alisema mgogoro huo anaujua na kuwa kukamatwa kwa watu wawili
katika kikao cha mkuu wa mkoa kulitokana na kutoka lugha chafu na kwamba
kutopakupata dhamana ni jukumu la mahakama.
Matei alitoa wito kwa watu wote ambao
wana matatizo kutoa taarifa kwa jeshi hilo na kwamba wao hawapo tayari kuona
mtu akionewa kwani kila mwananchi ana haki.
“Pamoja na mambo mengine nawashauri
wananchi wa Ipango kufuata taratibu kwa kusshirikisha viongozi wa husika katika
mgogoro huo lakini pia mbunge wao yupo wamtumie,” alisema.
0 comments:
Post a Comment