Salha Mohamed
SERIKALI kupitia Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeanza msako wa mikataba ya kampuni zinazotakiwa
kulipa kodi katika manispaa zake, ili kubaini ufisadi Dar es Salaam.
Hatua hiyo ya Serikali imefikiwa baada
ya kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, kulipa Sh milioni 687.9 kwa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kutokana na kuwapo madai ya ufisadi katika
ulipaji kodi.
Fedha hizo zililipwa Desemba 21 na ni za
kipindi cha miaka saba ambapo zilielekezwa katika ujenzi wa madarasa 40 katika
Manispaa hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi
alisema tayari Takukuru inafanya uchunguzi wa waliohusika kuficha mkataba wa
kampuni hiyo na kuisababishia Halmashauri kukosa mapato.
“Tumeanza msako na vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama, hatujali wanamlipa nani, watatulipa fedha zote wanazodaiwa
na Serikali haiwawekei kinga na mashitaka, vyombo vya ulinzi vinaendelea na
kazi yao nasi tunaendelea na kazi zetu,” alisema.
“Mkataba huo ambao haukuonekana kwenye
kumbukumbu za Manispaa kwa maana ya kuibiwa na kushindwa kutuwezesha Kinondoni
kupata mapato tangu mwaka 2009,” alisema.
Alisema alipata mkataba kutoka vyanzo
vyake na kuwataka kulipa kiasi hicho ndani ya siku saba, huku vyombo vya ulinzi
na usalama vikichunguza na kubaini mhusika aliyekuwa akilipwa fedha hizo,
aliyeiba mkataba na kuuficha.
Alitoa rai kwa kampuni zilizoingia
mkataba na Serikali anayedhani ameuficha au kuunyofoa kwenye kumbukumbu za
Manispaa walianza msako kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
Hapi alisema: “Takwimu zinaonesha mwaka
huu idadi ya wanafunzi 19,000 walifaulu Kinondoni, na kuchaguliwa awamu ya
kwanza ni 12,889 huku wanafunzi 3,169 wakikosa nafasi.”
Alisema wilaya ina upungufu wa vyumba
vya madarasa 79, ambapo vyumba 40 vitajengwa kwa fedha hizo na kubaki upungufu
wa 39.
Aliongeza kuwa watafanya tathmini ya
kuwa na sifa ya kujiunga na sekondari huku akibainisha kuwa hadi Januari wahakikishe
kila aliyefaulu anakwenda sekondari.
Hapi alisema: ”Nawaagiza wakurugenzi
wote mkoani humu wajipange ili kuhakikisha wanatimiza na kutekeleza maagizo ya
serikali yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Kila mtoto aliyefaulu anapata nafasi ya
kupata elimu ya sekondari, hili ni wajibu wetu, wakurugenzi na manispaa zote
kuhakikisha maagizo halali ya Majaliwa ili kuendelea kutekeleza nia njema ya Rais
John Magufuli,” alisema.
0 comments:
Post a Comment