Seif Mangwangi, Arusha
Godbless Lema na mkewewakiwa mahakamani |
RUFAA ya
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kupinga uamuzi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Arusha uliomnyima Mbunge huyo dhamana, imepangwa kusikilizwa Desemba
28.
Wakili
wa Lema, Sheck Mfinanga alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari
na kueleza kuwa rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi.
Kutokana
na hali hiyo ni dhahiri kwamba Lema atakula Krismasi akiwa mahabusu ya Gereza Kuu
la Kisongo ambapo Wakili Mfinanga alisema katika rufaa hiyo, watakuwa na hoja
sita za kupinga uamuzi huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Rufaa
hiyo itasikilizwa baada ya Mahakama hiyo Desemba 20 chini ya Jaji Modesta
Opiyo, kukubali maombi ya Lema ya kutaka kuongezewa muda kwa ajili ya
kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa ili isikilizwe.
Dk Opiyo
alitoa siku 10 kwa mawakili wa mbunge huyo kuwasilisha notisi hiyo ya kukata
rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha Novemba 11.
“Baada ya
kupitia kwa kina uamuzi wa Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi wa kukataa maombi yenu
ya rufaa kwa kuwa yalikuwa nje ya muda, nimebaini kwamba kulikuwa na siku mbili
za mapumziko, ambazo zilisababisha rufaa yenu kuonekana nje ya muda, kwa kuwa Mahakama
haifanyi kazi siku za mapumziko.
“Kutokana
na Mahakama kuridhishwa na sababu hizo, inawapa mawakili wa Lema siku 10 muwe
mmeshawasilisha notisi ya kukata rufaa," alisema Dk Opiyo, Desemba 20.
Baada ya
kauli hiyo, upande wa Serikali ukiongozwa na Mwanasheria Mwandamizi
Elizabeth Swai, akisaidiwa na Adelaide Kassela; ulikubaliana na uamuzi huo
pamoja na mawakili wa Lema; Mfinanga akisaidiwa na James Milya.
Awali maombi
hayo namba 69 yaliwasilishwa mahakamani hapo chini ya hati ya dharura na Wakili
Mfinanga chini ya kifungu 361(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Upande
wa utetezi uliamua kuwasilisha maombi ya kukata rufaa kutokana na kutoridhishwa
na uamuzi unaotarajiwa kukatiwa rufaa wa Novemba 11 kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, chini ya Hakimu Desderi
Kamugisha, ambako Lema anakabiliwa na kesi za uchochezi.
0 comments:
Post a Comment