Grace Gurisha
TAASISI ya Utawala Bora na MaendeleoTanzania (Cegodeta),
imeiomba Serikali kubadilisha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 haraka au kuifuta
kabisa kwa sababu inakinzana na Sheria ya Mtoto.
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Thomas Ngawaiya
alieleza kuwa sheria hiyo ilitakiwa ifutwe kutokana na kwamba inagongana na
Sheria ya Kimataifa ya Mwaka 2004 ambayo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania liliridhia kuwa mtu wa chini ya umri wa miaka 18 ni mtoto.
“Baada ya kupitisha sheria hiyo Bunge lilitakiwa
irekebishe Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, lakini halikufanya hivyo jambo ambalo
linaipa Mahakama wakati mgumu kwenye kuamua kesi za watoto wa chini ya miaka 18
kuolewa.
“Mahakama inaweza kuamua chochote kwa kuwa sheria
inaruhusu mtoto huyo kuolewa na hivyo kuchangia mimba za utotoni. Lakini hiyo
ni kinyume na haki za mtoto wa kike kwa sababu na yeye ana haki ya kusoma kama
mtoto wa kiume,” alisema Ngawaiya.
Alisema wanaishauri Serikali kuchukua hatua za makusudi
zinazolenga kufanikisha utoaji wa elimu kwa watoto wa kike wanaopata ujauzito
na kujifungua kabla ya kuhitimu masomo yao.
Pia, alisema wamefikia hatua hiyo kufuatia utafiti
iliyoufanya na kubaini changamoto mbalimbali zinazohitaji kutatuliwa kwa haraka
ili kujenga taifa lenye nidhamu kwa ngazi zote. Alisema hatua hiyo itawawezesha
wale waliokumbwa na mikasa ya ujauzito kurejea mashuleni, ambapo pia itakuwa ni
fursa nyingine ya kupata elimu ya malezi ya watoto wao.
“Ili mtoto huyu aliyejifungua arudi shuleni kuendelea na
masomo ni vyema kuwe na madarasa maalumu kwa ajili hiyo tu au zijengwe shule
moja moja kwa kila wilaya, zikiwalenga watoto hawa ili waweze kupata masomo ya
ziada ya malezi ya mtoto”, alisema.
Ngawaiya alisema idadi ya watoto wanaopata ujauzito shuleni
haizidi asilimia 10, hivyo ametaka kuwepo hatua za makusudi ili kupunguza idadi
hiyo, sanjari na kuendelea kutoa adhabu kali kwa wale wanaobainika kuwapa mimba
wanafunzi bila kujali nyadhifa zao.
0 comments:
Post a Comment