Venance Matinya, Mbeya
JESHI la polisi
mkoani Mbeya limewaua watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi katika
mapambano ya kurushiana risasi. Katika tukio hilo, jambazi mmoja alifanikiwa
kuwakimbia polisi hao.
Kamanda wa
polisi mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari amethibitisha hilo na kueleza kuwa
lilitokea juzi saa moja na dakika 45 jioni katika Kijiji cha Busisya, Kata
ya Kisiba, Wilaya ya Rungwe.
Alisema Askari
Polisi wa Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari Polisi Wilaya ya Rungwe kwa
walipata taarifa za siri za kuwepo kwa majambazi wenye silaha ambao walikuwa na
lengo la kufanya uvamizi katika duka la mfanyabiashara wa soda na bia za jumla
ambaye pia ni wakala wa M-Pesa.
Alisema baada ya
taarifa hiyo kupatikana, askari Polisi wa Mbeya na wale wa Wilaya ya Rungwe
walianza kuwafuatilia majambazi hao na muda wa saa 19:45 jioni katika barabara
ya Tukuyu – Mbambo, askari walikutana na majambazi hao wakiwa wamepakiana
katika pikipiki aina ya T- Better ambayo haina namba ya usajili yenye rangi
nyekundu.
Alisema baada
ya majambazi hao kugundua kuwa wanafuatiliwa na askari, walianza kuwarushia
risasi askari hao na ndipo yalipotokea majibizano ya risasi kati ya askari na
majambazi hao.
Alisema katika tukio
hilo bunduki tatu na risasi tisa zilizokuwa zinatumiwa na majambajhi hao
zilipatikana.
Alizitaja silaha
hizo kuwa bunduki aina ya Mark IV yenye namba 38482 na risasi mbili, Short
Gun Greener yenye namba G.73878 na risasi 1 na Gobole lililotengenezwa kienyeji
ambalo halina namba na risasi 6.
Aliongeza kuwa
baada ya kupekuliwa majambazi hao walikutwa pia na vitu vingine ambavyo ni
rungu moja, praizi moja, bisibisi moja, mafuta ya cherehani, koti la ngozi
rangi ya brown na begi dogo rangi nyeusi ambalo lilitumika kuhifadhi vitu
hivyo.
Kamanda
Kidavashari alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya
Serikali Makandana iliyoko wilayani Rungwe kwa uchunguzi wa kitabibu na kutambuliwa
na ndugu zao.
Alisema msako
unaendelea na kwamba katika tukio hilo hakuna mali iliyoporwa wala askari
kupata madhara, lakini jitihada za kumtafuta jambazi aliyekimbia bado
zinaendelea.
0 comments:
Post a Comment