Mary Mtuka
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),
kimetakiwa kuchangamkia fursa za kuandaa wataalamu wa kada mbalimbali za
usafirishaji wa anga, ili kuinua sekta hiyo na kuiwezesha nchi kujulikana
kimataifa.
Akizungumza Dar es Salaam juzi katika
uzinduzi wa Baraza la Chuo hicho, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa, alisema kuzalisha wataalamu pekee haitoshi.
Alifafanua kuwa ni jukumu la uongozi wa
Baraza hilo, kusaidia wataalamu hao kwa kuwaunganisha na mashirika makubwa ya
usafirishaji.
Profesa Mbarawa aliutaka uongozi wa Chuo
hicho kuweka mifumo imara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ili
kuwajengea mazingira mazuri walimu na wanafunzi.
Alisema lengo ni kuwajengea uwezo
wasafirishaji hao katika kuhakikisha wanatambulika kimataifa na kujitangaza
zaidi.
“Tayarisheni wataalamu na muwakutanishe
na wakurugenzi wakuu wa kampuni kama Emirates, Qatar na Etihad, ili muwawezeshe
kupata fursa kirahisi kwa kuonekana kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.
Alikitaka chuo hicho kuchukua
wafanyakazi kutoka Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kuwapa mafunzo ili
kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kujenga miradi, ikiwamo ya ujenzi
wa reli ya kisasa.
“Msipotumia fursa kama hizi kuandaa
wataalamu, tutakosa watalaamu wazawa wa miradi mikubwa na kuanza kulalamika
kuwa chuo kipo lakini hakithaminiki, kumbe mwanzoni tulishindwa kujipanga,”
alisema.
Profesa Mbarawa alisema Baraza
lililopita lilikuwa na uwezo wa kukusanya mapato ya ndani yatokanayo na ada za
wanafunzi kutoka Sh bilioni 2.1 mwaka wa fedha 2011/12 hadi Sh bilioni 5.1
mwaka 2015/16.
Pamoja na mafanikio hayo, aliutaka
uongozi kupunguza idadi ya kozi na kuwa na chache zenye tija na soko kimataifa,
ili kufanya chuo hicho kuwa cha kipekee Afrika.
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Zakaria
Mganilwa alisema chuo kitaendelea kuandaa wataalamu mahiri na waliobobea katika
sekta ya uchukuzi na usafirishaji na kuomba Serikali kuendelea kusaidia
kuboresha miundombinu yake.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa Bavon
Nchomba alimhakikishia Waziri kuwa changamoto zote zinazokabili chuo,
zitashughulikiwa kwa kuanzia na upunguzaji kozi zisizo na tija.
0 comments:
Post a Comment