Grace Gurisha
UPANDE
wa Serikali katika kesi ya Yusuf Yusuf (34), maarufu kwa jina la ‘Mpemba’ kuwa
ni kinara wa ujangili umejichanganya kwa kushindwa kuieleza Mahakama hatua
inayofuata, baada ya upelelezi kukamilika na kuishia kudai kuwa upelelezi
umekamilika.
Mgongano
huo ulitokea jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Thomas Simba wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipokuja kwa hatua ya
washitakiwa kusomewa maelezo ya kesi yakiwemo maelezo ya mashahidi.
Wakili
wa Serikali Elizabeth Mkunde aliieleza Mahakama kuwa uchunguzi wa kesi hiyo
umekamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa na kudai kuwa jarada la kesi
linaandaliwa kupelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kwa
sababu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kauli
hiyo ilimshtua Wakili wa upande wa utetezi, Nehemia Nkoko na kuanza kumbana
wakili huyo kwa kueleza kuwa tayari walishadai kuwa upelelezi umekamilika na
kwamba wanasubiri kuwasomea washitakiwa maelezo hayo au kibali cha kusikiliza
kesi hiyo katika Mahakama ya Kisutu, hivyo anashangaa Serikali kuja na hoja ya
upelelezi umekamilika.
Simba
alikubaliana na Nkoko kuwa awali walisema upelelezi umekamilika, na kuhoji kwa
nini jana wanatoa taarifa zilezile wakati yeye alisharekodi kuwa umekamilika,
kwa hiyo akamtaka wakili huyo aeleze hatua inayofuata.
Akijibu
hoja hizo, Mkunde alidai kuwa jarada la kesi hiyo lipo kwa Mpelelezi Mkuu wa
Kanda Maalumu tayari kwa kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kwa
hiyo hatua za awali za upelelezi zimekamilika.
Hakimu
aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 26, mwakani, ambapo ameutaka upande wa
serikali uje na majibu yanayoeleweke kwa sababu wanaichanganya Mahakama.
Awali,
Wakili wa Serikali Paul Kadushi alidai kuwa upelelezi umekamilika na hivi sasa
wanaandaa maelezo ya mashahidi na vielelezo kupeleka katika Mahakama Kuu
Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama mahakama ya
ufisadi.
Mbali na
Mpemba ambaye ni mkazi wa Tegeta washitakiwa wengine ni Charles Mrutu (37)
mkazi wa Mlimba mkoani Morogoro, Benedict Kungwa (40) mkazi wa Mbagala Chamazi,
Jumanne Chima (30) mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius Kulagwa
(46).
Washitakiwa
hao wanashitakiwa na kosa ya kujihusisha na mtandao wa ujangili na biashara ya
meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.
Ilidaiwa
kuwa katika tarehe zisizofahamika kati ya Januari 2014 na Oktoba 2016 wakiwa
maeneo tofauti Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara walijihusisha na mtandao
wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali vipande 50 vya meno ya
tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 mali
ya Serikali bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aliendelea
kudai kuwa katika shitaka la pili, Oktoba 26 mwaka huu, washitakiwa wakiwa
Mbagala Zakhem ndani ya Wilaya ya Temeke walikutwa na vipande 10 vya meno ya
tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vyenye thamani ya dola za Marekani 30,000 sawa
na Sh milioni 65.4.
Ilidaiwa
kuwa katika shitaka la tatu, Oktoba 27 mwaka huu, washitakiwa wakiwa Tabata
Kisukulu walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vyenye uzito wa kilo 11.1 vyenye
thamani ya dola za Marekani 15,000 sawa na Sh milioni 32.7, ambapo pia Oktoba
29 mwaka huu walikutwa na viapande 36 vyenye thamani ya dola za Marekani sawa
na Sh milioni 294.6 bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
0 comments:
Post a Comment