Waandishi Wetu
Dk John Magufuli |
WAKATI Rais John Magufuli akiendelea
kuteua makada na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa
watendaji katika Serikali yake, vyama vya upinzani nchini vimeonya kuwa utaratibu
huo unaweza kuzaa viongozi wanaotoa matamko na uamuzi wa kukilinda chama hicho
tawala badala ya taifa.
Aidha, vyama hivyo vimeeleza kwamba
jambo hilo ni matokeo ya kuwa na Katiba inayompa Rais madaraka makubwa,
vikitolea mfano baadhi ya wateule hao wanavyorumbana na wapinzani kila kukicha ambapo wamemshauri Rais
huyo kuteua zaidi wataalam wasiojipambanua kama wafuasi wa chama chochote cha
siasa.
Hata hivyo, akizungumza wakati wa
mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM hivi karibuni, Rais Magufuli alitetea
uamuzi wa kuteua wanaCCM kwenye nafasi mbalimbali akisema ndio watu
anaowafahamu na kwamba CCM ndiyo imepewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Katika mahojiano na JAMBO LEO kwa
nyakati tofauti, juzi viongozi wa vyama hivyo vya upinzani walisema kwamba licha
ya watumishi wa Serikali kuwa na itikadi tofauti za siasa, hawawezi
kulinganishwa na watendaji wengine wanaoingia Serikalini wakijulikana ni
wanachama wa CCM na wengine wanaotokea kwenye uongozi ndani ya chama hicho.
Juzi Rais Magufuli aliteua wakuu wa wilaya
wawili, wakurugenzi watatu wa Mamlaka za Serikali za mitaa na wenyeviti saba wa
Bodi za taasisi huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki
akiteua makatibu tawala wa wilaya 27 kujaza nafasi zilizokuwa wazi.
Lakini wanasiasa hao walidai kuwa uteuzi
huo ni mwendelezo ule ule wa siasa za CCM ambapo walimtaja Diwani wa Kata ya
Kiloka (CCM) Robert Selasela ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Kilombero
kuwa ni mfano wa watendaji hao.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo
Kairuki alisema: “Kwani sheria za madiwani zikoje? Mstahiki Meya Kinondoni
alipokuwa katika nafasi hiyo hujui kuwa alikuwa anafanya kazi TRA (Mamlaka ya
Mapato Tanzania).”
Katika maelezo yake Selasela alisema: “Udiwani
sio kazi ya kudumu, lakini pia nitaona wakubwa watakavyoshauri. Mambo haya yana
kanuni za utumishi na za viongozi. Nitaangalia miongozo yote na mwisho wa siku
nitafanya uamuzi sahihi ambao hautaathiri upande wowote. Ila kwa sasa mawazo
yangu yote yapo Kilombero.”
Wanasiasa
Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AFP),
Rashid Rai alisema: “Anachokifanya Rais ni kuteua watu watakaolinda maslahi
fulani na kupambana na wapinzani katika maeneo wanayoyaongoza.”
“Mfano ni Jimbo la Arusha, kuna mvutano
mkali kati ya Lema (Godbless-Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema) na Gambo
(Mrisho-Mkuu wa mkoa Arusha). Rais anasema yeye ni wa watu wote ila mbona
anateua wa chama chake tu?”
Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK),
Renatus Muabhi alisema: “Wanapelekwa zaidi katika maeneo ambayo wapinzani wana
nguvu ili wakapambane nao na kumaliza nguvu zao za kisiasa.”
Huku akitolea mfano wa Jimbo la Arusha,
Muabhi alisema kada wa CCM akiwa Katibu Tawala hawezi kukubali kupitisha jambo
linaloonekana wazi kukiminya CCM, hata kama lina maslahi katika sehemu husika.
Alifafanua: “Yamekuwa mazoea kwa awamu
zote kuwa na watu wa aina hii ili kuvunja upinzani. Lazima aweke watu wa chama
chake, tena baadhi ndio wanaokuja kuwa wasimamizi wa changuzi mbalimbali.”
Alisema ni vigumu kuwa na uhusiano mzuri
kati ya wateule hao wa Rais na wabunge wa upinzani katika maeneo mbalimbali
nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama
cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema: “Tumefikia hapa kutokana na kuwa na
Katiba mbovu ambayo inampa Rais mamlaka makubwa bila mtu mwingine kuhoji, kwa
mfano uteuzi wa makatibu hawa haujabainishwa wazi wanapaswa kuwa na sifa zipi
bali kama mteuzi anaridhika nao anaweza kuwachagua.”
Alidai kwamba baadhi ya wateule hao huwa
vinara wa kuharibu chaguzi mbalimbali huku akitolea jinsi wakurugenzi wa
halmashauri walivyovuruga chaguzi za mameya, ukiwemo wa Meya wa Kinondoni.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda
Juju aliungana na Mtatiro huku akitaja maeneo ambayo wateule hao wa Rais
wanalumbana na wabunge na madiwani wa upinzani.
Ends
0 comments:
Post a Comment