Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es
Salaam, Desemba 7 inatarajia kutoa uamuzi wa maombi ya upande wa utetezi katika
kesi ya kuvua samaki bila kibali, maarufu kama ‘Samaki wa Magufuli’ ya kutaka
warudishiwe meli ya Tawaqar I, tani 296.3 za samaki na Sh bilioni 2.
Kesi hiyo, ilikuwa ikiwakabili raia
wawili wa China, Hsu Tai na Zhao Hanquing ya kuvua samaki kwenye bahari ya
Hindi bila kibali.
Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani
hapo na mawakili Kapteni Bendera na John Mapinduzi, ambao wanadai mmiliki wa
mali hizo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Al Araim Sea Tawaqar LLC Oman, Said Ali
Mohamed.
Mawakili hao walifikia uamuzi huo, baada
ya raia hao kushinda rufaa waliyokata kupinga adhabu ya kifungo jela.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP), Biswalo Mganga aliwasilisha pingamizi la awali akiiomba Mahakama
kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu yana upungufu kisheria.
Wakili wa Serikali Mkuu,Timony Vitalis
alieleza mbele ya Jaji Ama-Isario Munisi kuwa anapinga maombi hayo kwa sababu
tayari kesi hiyo ilikwishatolewa hukumu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar
es Salaam ikiamuru Serikali kulipa meli ya uvuvi na samaki waliokamatwa miaka
mitano iliyopita.
Alidai kwamba inashangaza kuona upande
wa utetezi unamtaja Mohamed kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli hiyo na kwamba
haijampa mali zake, wakati si mmiliki.
Vitalis aliendelea kudai kuwa hukumu ya
Kisutu ilishafutwa na Mahakama ya Rufani ambayo iliwaachia huru baada ya
kushinda rufani yao, hivyo Mahakama Kuu haina mamlaka tena ya kujiwezesha kumjua
mmiliki halali.
“Kama kesi ilishafutika na vielelezo
vikarudishwa kwa wahusika, utaiombaje Mahakama imtambue mmiliki wa mali hizo?” Alihoji.
Pia alibainisha kwamba meli hiyo haiko
mikononi mwa Mahakama hiyo, hivyo kwa sasa haina mali hizo kutokana na hukumu kutolewa.
Kutokana na mvutano wa kisheria na hoja,
Jaji Munisi aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 7 atakapotoa uamuzi.
Februari 23, 2012 Mahakama Kuu
iliwahukumu Hsu na Zhao kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kuwatia
hatiani kwa kufanya uvuvi haramu.
Machi 28 mwaka huu, Mahakama ya Rufani
iliwaachia huru baada ya kushinda rufani yao ya kupinga adhabu ya kifungo hicho
au kulipa faini ya Sh bilioni 20 iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam.
0 comments:
Post a Comment