Peter Kimath, Morogoro
MKAZI wa Kijiji cha Dodoma Isanga Kata
ya Masanze wilayani Kilosa, Agustino Mtitu amepigwa mkuki mdomoni na kutokea
upande wa pili wa shingo na wafugaji akiwa katika harakati za kuzuia mifugo
iliyoingia shambani na kula mazao.
Diwani wa Kata ya Msanze, Bakari Kilo alisema
kuwa Desemba 25 mwaka huu, majira ya saa 3:00 asubuhi alipigiwa simu na
wananchi akielezwa kuwa kuna mifugo imeingia katika Kijiji cha Dodoma Isanga na
kuharibu mazao shambani.
Bakari alisema wakulima wakiwa wanazuia
ngo’mbe kula mazao, ndipo lilipotokea kundi la wafugaji na kuanza kulumbana na
wakulima hao.
Wakiwa kwenye majibazano, mfugaji mmoja
alimpiga Agustino Mtitu mkuki wa mdomoni.
Alisema Mtitu alipelekwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa matibabu, lakini walishindwa kumtibu jeraha
hilo na alisafirishwa kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu
zaidi.
Alisema wakiwa katika harakati za
kushughulikia mgonjwa huyo, wakulima walizuia mifugo ya wafugaji ili ajitokeze
mwenye mali lakini walishindwa kufutia kundi la wafugaji kufika eneo na kuanza
kuwashambulia.
Aliwataja walioshambuliwa na kupelekwa
katika Hospitali ya Wilaya Kilosa ni Yohana Wise, Josephati Mtitu, Paulo
Thomas, Mathayo Elias na George Andrea, hali zao zinaendelea vizuri.
Bakari aliwataka wafugaji kuheshimu maeneo
ya wakulima na kwenda kwenye maeneo yao, huku akiomba jeshi la polisi
kuwachukulia hatua waliofanya vurugu hizo.
Kwa upande, Daktari wa Hospitali ya Mkoa
wa Morogoro, Dk Frank Jakobo alisema Desemba 25 majira ya saa 10 jioni,
walipokea mgonjwa aliyetambulika kwa jina la Agustino Mtitu kutoka Hospitali ya
Wilaya ya Kilosa akiwa na mkuki mdomoni.
Dk Frank alisema hali ya mgonjwa huyo
inaendelea vizuri na walifanikiwa kumtoa mkuki huo mdomoni tangu juzi na sasa
anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari.
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mikumi kupitia
katibu wake, Robert Galamona imelaani kitendo kilichofanywa na wafugaji hao na
kuiomba Serikali kuwabaini waliofanya kitendo hicho cha kinyama.
Galamona alitaka wahusika wapewe adhabu
kali kwa mujibu wa sheria na ili iwe fundisho kwa wananchi wenye tabia ya
kujichulia sheria mkononi pindi inapotokea kutofautiana kati ya pande mbili.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa
Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha tukio hilo na kusema bado jeshi la polisi
linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria.
Wilaya ya Kilosa na Mvomero mkoani
Morogoro zimekuwa vinara kwa vurugu za
wakulima na wafugaji kwa miaka mingi na hadi sasa hakujawa na suluhu ya kudumu
iliyopatikana kuhusu migogoro hiyo.
0 comments:
Post a Comment