UTAFITI wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya
Maralia, umebaini kuwa asilimia 81 ya kaya zote nchini hazina choo bora, huku
wanawake wanaoishi mjini, wakikutwa na unene uliopindukia kwa asilimia 42.
Akizindua matokeo ya utafiti huo jana, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema matokeo hayo
hayaoneshi picha nzuri na hayaleti matumaini katika nchi.
Mbali masuala ya choo na unene, utafiti huo uliotolewa na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umeonesha kuwa mimba za utotoni nazo
zimeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi asilimia 27, 2016/17 kwa watoto
wa miaka 15 hadi 19.
Kutokana na matokeo hayo, Ummy alisema Serikali
inatarajia kuanzisha mpango maalumu wa kupambana na 'mafataki', ili kupunguza
tatizo la kuongezeka kwa mimba za utotoni.
Alisema hiyo ni changamoto kwa Serikali na wadau wanaopaswa
kukabiliana nayo kwa kuwaandaa watoto waendelee na masomo, huku akisema Serikali
itaendelea kutoa elimu juu ya madhara yanayoweza kujitokeza kwa wasichana kuzaa
wakiwa wadogo.
"Hili suala la kupambana na mafataki nitalibeba na
kulisimamia, ili kuondoa tatizo hilo na kutoa nafasi kwa watoto wakike
kuendelea na masomo kwani elimu ndio mkombozi pekee wa watoto hao,"
alisema.
Kuhusu vyoo, utafiti huo ulionesha kuwa ni asilimia 19 tu
ya Watanzania wote ndio wanaotumia vyoo vilivyo bora; vijijini asilimia 10 huku
mijini kukiwa na asilimia 35.
Kuhusu hali hiyo, Ummy alisema Serikali haiwezi
kukubaliana na suala hilo na kuzitaka kaya hizo kuhakikiha zinakuwa na vyoo
bora.
"Haiwezekani miaka 55 ya Uhuru bado wapo Watanzania
wanaojisaidia katika vichaka na maeneo yasiyo sahihi. Hii ni miongoni mwa
sababu nyingine ya kuongezeka kwa kipindupindu hivyo suala hili nitalibeba na
kulishughulikia," alisema.
Alisema tayari ametoa maelekezo kwa kila kaya kutumia
choo bora, hivyo ikifika 2017 Juni atakayekuwa na kaya isiyo na choo bora,
atafikishwa mahakamani.
Aliongeza kwua hawezi kuwa waziri wa kutoa matamko kuhusu
kipindupindu, wakati kuna watu hawataki kujikinga ikiwemo kwa kujenga vyoo
bora.
Kuhusu unene, utafiti huo ulibainisha kuwa katika kila
wanawake 100, 28 wana unene uliopindukia na kwa mijini, asilimia 42 ya wanawake
ndio wenye hali hiyo ikilinganishwa na vijijini ambako wanaokabiliwa na tatizo
hilo ni asilimia 21.
Ummy alishauri wanawake kujenga utaratibu wa kufanya
mazoezi ya mwili ili kupunguza tatizo hilo kwani ni changamoto.
Akitoa taarifa fupi ya utafiti huo, Mwakilishi kutoka
NBS, Sylvia Meku alisema utafiti huo ni wa sita kufanyika katika maeneo 608
nchini, ambapo kila eneo umefanyika katika kaya 22.
0 comments:
Post a Comment