Waandishi Wetu
Mwalimu Julius Nyerere |
TANGU Tanzania ipate uhuru imekuwa na
mawaziri wakuu 15, lakini miongoni mwao wapo waliojitosa kuwania urais bila
mafanikio, huku wachambuzi wakitaja sababu 13 zinazofanya washindwe. Waziri
Mkuu pekee aliyefanikiwa kuwa rais ni Julius Nyerere.
Miongoni mwa sababu za kushindwa
mawaziri hao ambazo zilitolewa na wachambuzi ni pamoja na kitendo cha mawaziri
hao kutetea hoja na mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali.
Kwa mujibu wa wachambuzi hao, kitendo
hicho kinawafanya waonekane hawana jipya kwa kuwa mara nyingi Serikali
inayomaliza muda wake huondoka na lawama nyingi.
Baadhi ya mawaziri wakuu waliojitosa
kuwania urais na kuishia katika ngazi za awali ama mchujo ndani ya CCM ni
Edward Lowassa ambaye jina lake likakatwa na Kamati Kuu na CCM na baadaye akaamua kuhamia Chadema ambako
aligombea kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na Ukawa katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015.
Licha ya kushindwa, mara kadhaa Lowassa
ameeleza kuwa uchaguzi huo haukuwa wa
haki na kubainisha kuwa atagombea tena mwaka 2020.
Wengine ni Salim Ahmed Salim, Mizengo
Pinda, John Malecela, Frederick Sumaye na Cleopa Msuya.
Walichosema wasomi
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema sababu ya
kwanza ni kusaka mgombea ambaye anajiuza kwa wananchi, bila kujali nafasi yake
serikalini ndio sababu ya kukatwa kwa majina ya wagombea katika mchujo ndani ya
CCM.
Alisema hiyo haina maana kuwa mawaziri
hao walikuwa na makandokando, bali walizidiwa vigezo na wagombea wengine, hivyo
majina yao kukatwa. Alisema vigezo vinavyotumika ni uwezo na uzoefu katika
uongozi, uadilifu, unyenyekevu na busara.
Pia, elimu ya chuo kikuu au inayolingana
na hiyo, mtu mwenye upeo mkubwa wa kuimarisha na kuendeleza Muungano, umoja na
amani.
Alisema vigezo vingine ni kuwa mtetezi
wa wanyonge na haki za binadamu na mtu asiye na
tamaa ya kujipatia umaarufu, kuzifahamu, kuzitetea na kutekeleza sera na Ilani ya CCM, mpenda haki
na ajuaye kupambana na dhuluma, kutokuwa mtu
mtu anayetumia nafasi ya uongozi kujilimbikizia mali.
Alisema kanuni za uteuzi wa wagombea
katika Vyombo vya Dola, zinazoendelea kutumika ni zile zilizopitishwa na
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ya mwaka 2010.
“Wananchi wanapenda mabadiliko ya
uongozi, hivyo tabia ya kujiibua badala
ya kuibuliwa ni tatizo, Lowassa hali
hiyo itaendelea kumtesa hata 2020,” alisema.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Nestory
Kobelo alisema waziri mkuu ni mtendaji wa shughuli za kila siku za serikali,
Rais anaposafiri nchi inakuwa chini yake.
Alisema rais anapokosea suala lolote la
kiutendaji, waziri mkuu ndiyo aliyeshindwa kumshauri vizuri ili atekeleze
wajibu wake wa kuwatumikia wananchi.
“Rais anapomaliza kipindi chake ya
uongozi wa miaka 10 na jina la waziri
mkuu hubadilika na kuitwa mstaafu wa serikali iliyopita,”alisema.
Alisema uwajibikaji katika ngazi za
chini kitatumika kama kigezo namba moja katika changuzi ndani ya CCM na siyo
nafasi ya mtu.
Mchambuzi wa masuala ya siasa,
Abdulkarim Atiki alisema mfumo wa CCM hauzingatii nafasi ya mtu serikalini,
hivyo hawawezi kumchangua mtu ambaye utendaji wake unafahamika.
Alisema CCM wanaogopa kuchagua waziri
mkuu kwani kama kulikuwa na dosari katika utawala uliopita, wananchi watasema
ni utawala uleule hakuna mabadiliko.
“Tanzania imejijengea sifa kwa kuibua
marais kutoka ndani ya baraza la mawaziri tangu Awamu ya Pili hadi Awamu ya
Tano,” alisema.
Mhadhiri mwingine wa UDSM Profesa Kitila
Mkumbo alisema Msuya aliwahi kufikia tatu bora katika kinyang’anyiro cha urais
mwaka 1995.
“Unajua kinyang’anyiro hicho kilikuwa
kikali baada ya Msuya kupenya, Rais mstaafu Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete
na baadaye Mkapa akaibuka kidedea kuwa Rais,” alisema.
Historia ya mawaziri wakuu
Desemba 9, 1961 Nyerere alikuwa Waziri
Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Tanganyika kabla ya kujiuzulu na kumwamchia
wadhifa huo, Rashid Kawawa ambaye aliteuliwa Januari 22, 1962 na kushika
wadhifa huo hadi Desemba 1, 1962.
Kawawa aliteuliwa tena kushika wadhifa
huo Februari 17, 1972 hadi Februari 13,
1977 na baada ya kung’atuka nafasi yake ilichukuliwa na Edward Sokoine.
Sokoine alishika nafasi hiyo ya mtendaji
mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1977 hadi
1980 na kupokewa na Msuya aliyedumu
katika wadhifa huo kuanzia mwaka 1980 hadi 1983.
Mwaka huo huo, Sokoine alirejea tena na
kudumu kwa takribani miezi 14 mpaka Aprili 12, 1984.
Wiki mbili baadaye, yaani Aprili 24,
1984, Dk Salim aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa tano na kudumu katika nafasi hiyo
hadi Novemba, 1985.
Mwaka huohuo, Jaji Joseph Warioba
aliteuliwa kushika wadhifa huo hadi mwaka 1990. Baada ya Jaji Warioba
kung’atuka nafasi yake ilichukuliwa na John Malecela ambaye alikuwa Waziri Mkuu
kuanzia mwaka 1990 hadi Desemba 7, 1994.
Msuya alirejea katika wadhifa huo
Desemba, 1994 hadi Novemba 1995.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995,
Frederick Sumaye aliteuliwa kushika wadhifa huo. Sumaye ndiye Waziri Mkuu pekee
aliyedumu katika nafasi hiyo kwa miaka yote kumi.
Mwaka 2005 Lowassa aliteuliwa kuwa
Waziri Mkuu na kudumu kwa miaka mitatu
hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu kutokana na kashfa ya kampuni ya Kufua Umeme
ya Richmond. Baada ya kung’atuka, nafasi yake ilichukuliwa na Mizengo Pinda
mpaka mwaka 2015.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,
Kassim Majaliwa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu nafasi anayodumu nayo mpaka sasa.
0 comments:
Post a Comment