Milioni 300/- zaliwa Mtwara Mikindani

Sijawa Omary, Mtwara

Suleiman Jafo
ZAIDI ya Sh milioni 300 za Manispaa ya Mtwara Mikindani zimepotea katika matumizi yasiyokuwa sahihi.

Hayo yalibainishwa jana kwenye ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sulemani Jafo mkoani hapa.

Fedha hizo zilitakiwa kutumika kwa ujenzi wa sekondari za Manispaa hiyo.

Kwa upotevu huo, Naibu Waziri alitoa agizo kwa uongozi wa Manispaa kuchukua hatua mara moja dhidi ya wahusika wa ubadhirifu huo kwani kitendo hicho kinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

“Hatuwezi kuvumilia mazingira kama haya, ni lazima hatua zichukuliwe wafikishwe mahakamani, hatuna mjadala,” alisema Jafo na kuongeza: “Hata kama wanasiasa wamehusika na hili wachukuliwe hatua.”

Katika taarifa ya hiyo iliyosomwa na Mkuu wa Sekondari ya Umoja, Beatrice Masanja kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa, Beatrice Dominic ilielezwa kuwa mwaka wa fedha 2015/16 Halmashauri ilipokea Sh 457,875,867 kwa stakabadhi namba 261503 kutoka kwa Katibu Mkuu Hazina kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule hizo zikiwamo Chuno, Shangani na Umoja.

Aidha, Mkurugenzi alisema baada ya kugundua upotevu huo hatua aliyochukua ni kuwasimamisha kazi wahusika wa tukio hilo ili kupisha uchunguzi.

Miongoni mwa utekelezaji wa majukumu yake, mkoani hapa ni kuzungumza na watumishi wa halmashauri zote za mkoa huu na kutembelea sekondari ya Umoja na mradi wa dampo wa Mangamba.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo