Abraham Ntambara
WAFANYABIASHARA nchini wametishia kuacha kazi hiyo rasmi
na kufanya shughuli za kimachinga kama Serikali haitatenga haraka maeneo ya wafanyabiashara
wadogo kwa kuwa wanapata hasara kwa kukosa biashara huku wakilipa kodi.
Kauli hiyo imekuja baada ya hivi karibuni Rais John
Magufuli kuamuru wamachinga wasibughudhiwe, waachwe wafanye biashara zao katika
maeneo ya mijini.
Akizungumza jana Dar es Salaam na JAMBO LEO, Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja alisema wafanyabiashara
wenye maduka wanaweza kuingia katika mfumo huo ili kuepuka kodi.
“Wafanyabiashara wanaweza kuacha shughuli hiyo rasmi na
kuwa wamachinga, kwa sababu wanatambua kwamba
hawatawajibika kulipa kodi ya Serikali,” alisema Minja.
Aidha, aliitaka Serikali kuchukulia suala hilo kwa uzito,
kwa kuwa wafanyabiashara wanatumia mashine za elektroniki (EFDs) ambao
wanatakiwa kuonesha mauzo yao na kuangaliwa wasiendelee kupata hasara kutokana
na wamachinga kwani kunafanya wasipate wateja na hivyo kukosa faida.
Minja aliongeza kuwa wafanyabiashara wengi wanaofanya
shughuli za kibiashara kihalali wangependa kutumia njia isiyo rasmi kama ya
wamachinga, kwa kuwa kuna mteremko fulani wa kutolipa kodi ambao unawafanya
wapate faida zaidi.
Alisema kuruhusu wamachinga kufanya shughuli zao karibu
na maduka si sahihi, kwani alibainisha kwamba wanatakiwa kutengewa maeneo ambayo yao ambayo watakutana na
wateja wao.
Minjua alisema anaamini kuna wateja wa wamachinga, wa
madukani na wa maduka makubwa, hivyo mteja wa wamachinga hatarajii kuona mteja
wao akienda kununua mahitaji yake dukani.
Aliitaka Serikali kufanya utekelezaji wa haraka kutenga
maeneo ya wamachinga ili kila mfanyabiashara aweze kuwa eneo ambalo atakutana
na kuhudumia wateja wake.
Minja alisema walifanya mkutano na Waziri wa Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa moja ya ajenda ikiwa ni jingo la Machinga Complex
kuondolewa mikononi mwa waliopewa umiliki wa awali ili wamachinga wakafanyie
shughuli zao hapo kwa utaratibu wa kulipa kodi jambo ambalo halijatekelezwa.
0 comments:
Post a Comment