Humphrey Polepole |
MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Profesa Mwesiga Baregu, amemshauri Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya
CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kupeleka mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kwenye ngazi za juu za chama huku Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu
Joseph Warioba akisema hana la kusema.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya
Polepole kueleza kuwa licha ya kukubali madaraka ya usemaji wa chama hicho,
msimamo wake kisera wa Muungano wa Serikali Tatu unaopingana na matakwa ya
chama hicho ambao ni wa Serikali Mbili uko palepale.
Akizungumza na JAMBO LEO jana, Profesa
Baregu alisema ipo haja kwa Polepole kutumia fursa aliyopata kuishawishi CCM na
kuieleza kiundani kuwa mapendekezo ya Tume yalikuwa na maana kubwa, hivyo kama
anataka Muungano uendelee na uwe wa hiari na huru, mapendekezo yaliyopendekezwa
yalikuwa na misingi hiyo.
"Hivyo anayosema Polepole, atusaidie
ayachukue kuyapeleka hadi kwenye uongozi wa chama wa ngazi za juu, awaeleze
wayaelewe ili mchakato wa Katiba mpya umalizike ukiwa na maoni ya wananchi,"
alisema.
Alisema mapendekezo ya Katiba ya Bunge Maalumu
hayana maana yoyote kupigiwa kura ya ndio au hapana, kwa kuwa yalishatoka na
hivyo kinachotakiwa ni maoni yaliyotolewa na wananchi wenyewe, kwa kufuata Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwenye
Rasimu ya Jaji Warioba.
"Kuna watu hawaamini kama mapendekezo
yalitokana na wananchi, hivyo inabidi watambue kuwa lengo la Tume si kuvunja Muungano
bali kuuboresha na kuuimarisha," alisema Profesa Baregu.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu
Nyerere, Joseph Butiku ambaye alikuwa mjumbe wa Tume hiyo, alisema anachofanya
Polepole kwa sasa, basi kinachosubiriwa ni Katiba kupigiwa kura na tangu
wakubaliane kuhusu suala hilo, hakuna aliyekiuka maagizo.
Chadema
Mkurugenzi wa Itikadi, Itifaki, Uenezi,
Mawasiliano na Mambo ya Nje, Chadema John Mrema alimpa pole Polepole kwa kupewa
kazi ya kukisemea chama ambacho hakubaliani na misimamo yake kisera, huku
akitolea mfano suala la Katiba Mpya hasa ikizingatiwa kuwa moja ya misimamo
yake ni serikali tatu kinyume na msimamo wa CCM ambao ni wa serikali mbili.
Mrema alisema Polepole amepewa kazi ya
kukisemea chama ambacho hakijui, kwani hana rekodi ya kukulia ndani ya UVCCM au
kuwa na nafasi yoyote zaidi ya hivi karibuni kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya,
hivyo amekubali kukisemea chama ambacho hakijui, “hivyo atasema nini?
Akizungumzia mabadiliko ya ratiba za
vikao vya ndani ya CCM alisema ni dalili za wazi kuwa wamepoteza mvuto na
hawana ajenda za kujadili, hivyo kuamua kuongeza muda wa vikao ili wapunguze
kuhojiwa kwa Serikali yao ambayo hadi sasa imesababisha maisha kuwa magumu
zaidi kwa Watanzania, hata wanachama wao wanaisoma namba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Benson Bana alisema alichosema Polepole ni kuwa kwenye utendaji wake
atakubaliana na kitakachoamuliwa na chama hicho kwenye vikao na mikutano ingawa
msimamo wake utabaki palepale.
0 comments:
Post a Comment