Bahati Othmani, Hai
TAMAA ya kupata mali kwa baadhi ya
makabila imeelezwa kuwa ni sababu kuu ya kuendelea kuongezeka kwa tatizo la
mimba na ndoa za utotoni.
Suala hilo pia limeelezwa kuchangia
watoto wa kike kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Kauli hiyo imetolewa na washiriki wa
mafunzo ya mradi wa majaribio wa kukabiliana na mimba na ndoa za utotoni
unatekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Action For Justice in Society
(AJISO) katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro
Kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo
hayo walieleza kuwa tatizo hilo bado ni sugu na zinahitajika jitihada za
makusudi kulidhibiti kwa faida ya jamii.
Anna Samweli alisema kuwa tamaa ya fedha
na mali imekuwa chazo kikuu cha watoto wa kike kupata mimba na ndoa za utoto
kutokana na baadhi ya wazazi kuwalazimisha watoto hao kuolewa katika umri
mdogo.
Mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto
kutoka kituo cha polisi Bomang’ombe, Happynes Eliufoo alisema tatizo la mimba
katika wilaya hiyo linaendelea kuongezeka kutokana na baadhi ya wazazi
kushindwa kutoa ushirikiano pindi tatizo hilo linapotokea pamoja na kuficha
wanaohusika na matukio hayo
Alisema kuwa kwa kutumia kamati za
ulinzi na usalama wa mtoto kwa kila kijiji pamoja na jamii katika kupaza sauti
kwa lengo la kutetea na kulinda haki za watoto wa kike , ni njia nyingine nzuri
katika kukabiliana na vitendo hivyo mitaani.
“Ni vema wananchi wote kuunganisha nguvu
katika kusaidia kamati hizo zinafanya kazi ipasavyo kwa kutoa taarifa na kuacha
tabia ya kuwafungia ndani watoto wanapofanyiwa vitendo hivyo, huku wengine
wakimalizana wenyewe bila kufikishwa katika vyombo vya sheria”alisema Elifoo.
Kwa upande wake mwezeshaji kutoka Asasi
ya elimu mwangaza Tanzania inayojihusisha na masula ya ukatili dhidi ya watoto,
Michael Reubeni aliwataka washiriki wote kulinda watoto wa kike kwani
wanaofanya vitendo hivyo wako katika familia, majirani na hata wakati mwingine
walimu ambao wamepewa dhamana ya kukaa na kuwalinda watoto.
Alifafanua kuwa ili mradi huo uweze
kufanikiwa ni lazima viongozi wote kwa pamoja kutumia kauli mbiu ya mradi ya
“Tokomeza ndoa na mimba za utotoni hali ambayo itasaidia kuondoa unyanyasaji
huo utapungua kwa asilimia kubwa.
Ni wajibu wa kila mmoja kuona ana jukumu
la kusaidia utekelezaji wa mpango huu katika maeneo yake kama walivyoahidi
mawaziri na kwa umoja ni dhahiri vitendo hivi vitakomeshwa na kuwalinda watoto.
Msimamizi wa mradi huo kutoka AJISO,
Tatu Mruthu alisema kuwa lengo la kuongeza uelewa na stadi juu ya masuala ya
afya ya uzazi kwa vijana wa kike ili wajikinge na mimba za utotoni, UKIMWI na
tabia hatarishi hatimaye wamalize masomo yao salama.
Mruthu alisema unatekelezwa katika kata
mbili wilayani hapa ambazo utafiti ulionyesha kuwa tatizo la mimba na ndoa za
utotoni bado ni tatizo kubwa ambapo kwa awamu ya kwanza utatekelezwa katika
vijiji vya Sanya Stationi,Tindigani kata ya KIA na vijiji vya Chemka na
Rundugai kata ya Masama Rundugai
0 comments:
Post a Comment