Mwandishi Wetu, Dodoma
MFUKO wa Kuendeleza Hifadhi za Wanyamapori Afrika (AWT)
umeahidi kusaidia upatikanaji wa Sh bilioni moja ili kutekeleza awamu ya kwanza
wa kuimarisha mtandao wa Taasisi ya Huduma za Usafirishaji wa Pikipiki na
Bajaji (Tamosa).
Upanuzi wa mtandao huo unahusisha mikoa ya Dodoma, Mara,
Morogoro, Singida na Arusha.
Ofisa Mkuu Mwandamizi wa AWT, Pratik Patel alisema hayo
hivi karibuni mjini hapa, kwenye mkutano wa Bodi ya Wadhamini wa Tamosa ambapo pia
mikoa hiyo ilitajwa.
Mbali na kuongoza AWT, Patel pia ni mwakilishi wa taasisi
za kimataifa za hifadhi ya mazingira zikiwamo za World Conservation Fund na
African Wildlife Trust, zinazoendesha kampeni za kitaifa na kimataifa
kuendeleza utalii na kudhibiti ujangili dhidi ya tembo.
Alisema waendesha bodaboda hawapaswi kuachwa nje ya
mikakati ya kukuza uchumi wa Taifa, badala yake unahitajika usimamizi thabiti,
mafunzo ya sheria za usalama barabarani na kuboresha huduma za usafiri huo.
“Bodaboda wanagongwa, wanapoteza viungo, wanakufa...AWT
tutakaa na mshirika wetu, Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na Tamosa
kuangalia vipaumbele ili kuibua miradi ya kibiashara, elimu na uendeshaji wa
bodaboda kwa usalama na kukuza uchumi wa Taifa,” alisema.
Kwa mujibu wa Patel, mkakati huo utahusisha Serikali ili
kuchagiza kasi ya uboreshaji huduma za usafiri kwa kuendeleza madereva ili
pamoja na mambo mengine, waipende na kuiheshimu sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa Tamosa, Kizito Msangya alisema kama
ushirikiano uliopo kati yao na mamlaka kama halmashauri za wilaya, manispaa na
majiji, Polisi, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) utaboreshwa, kutakuwa na ufanisi wenye tija kwa pande
zote.
Msangya alisema katika kujiimarisha na kuboresha huduma
zao, Tamosa inakusudia kusajili vituo vya bodaboda, kuanzisha miradi na kutoa
mikopo ikiwamo ya pikipiki, ujenzi wa vituo vya mafunzo ya udereva na sheria za
usalama barabarani, ili kuwajengea uwezo madereva na kupunguza ajali
barabarani.
Mlezi wa Tamosa, Balozi Job Lusinde alisema kuwapo kwa
bodoboda ni matokeo ya uamuzi wa Serikali kufungua fursa pana za ajira hasa kwa
vijana.
“Hatua hii ilifungua mianya ya kibiashara ikiwamo soko la
watengenezaji na wauza pikipiki na kuimarisha huduma ya usafiri wa haraka kwa
nauli nafuu," alisema.
Lusinde alisema baada ya vijana wa Tamosa kufanya utafiti
wa kina, ilionekana umuhimu wa kuunda taasisi hiyo na kupitia malengo ya Katiba
yao, aliamua kuwaunga mkono na kuwa mlezi wao.
Mjumbe wa Bodi ya Tamosa kwa mkoa wa Dar es Salaam,
Gaudens Mushi alisema ushirikiano baina ya taasisi hiyo na kampuni za
kibiashara zikiwamo za mawasiliano ya simu za mkononi, utasaidia kuanzisha na
kuendeleza kampeni ya elimu ya usalama barabarani.
0 comments:
Post a Comment