Watoto 61 wazaliwa Mkesha wa Krisimasi

Hussein Ndubikile

WATOTO 61 wamezaliwa usiku wa mkesha wa Sikukuu ya Krismasi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na hospitali za rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam za Amana, Temeke na Mwananyamala. Kati ya watoto hao, watoto 30 ni wa kiume na wengine 31 wa kike.

Ofisa Muuguzi wa zamu wa Jengo la Wazazi la MNH, Amina Kidavashari alisema watoto tisa walizaliwa katika mkesha huo ambapo kati yao wa kike ni wanne na wa kiume ni watano. “Watoto tisa wamezaliwa usiku wa kuamkia leo (jana) wanne wa kike na wa kiume watano idadi ya wazazi wanaokuja kujifungulia hapa Muhimbili imepungua sababu ya kuwapo hospitali za rufaa zinazotoa huduma ya uzazi,” alisema.

Alisema watoto watano walizaliwa kwa njia ya operesheni na wanne walizaliwa kwa njia ya kawaida.

Muuguzi Kiongozi wa zamu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana, Theresia Akida alisema wataoto 28 walizaliwa hospitalini hapo na kati yao wa kiume ni 16 huku wa kike wakiwa 12 na kwamba wawili pekee ndio waliozaliwa kwa operesheni.

Kwa upande wake, Ofisa Muuguzi wa zamu wa Hospitali ya Mwananyamala, Zulfa Julla alisema watoto 16 wamezaliwa mkesha wa Krisimasi na kwamba idadi ya watoto wa kiume na wa kike ni sawa kwani kila jinsi wamezaliwa watoto wanane. Naye, Ofisa Muuguzi wa Temeke, Hamisa Thabiti alisema watoto wanane walizaliwa na kati yao wa kiume mmoja.

Hamisa alisema miaka ya nyuma hospitali hiyo watoto kati ya 30 hadi 45 walikuwa wakizaliwa na kufafanua kuwa idadi hiyo imepungua kutokana na kuwepo kwa vituo vya afya katika maeneo ya pembezoni mwa wilaya hiyo.

Aliongeza kuwa maeneo kama vile Mbagala kwa sasa wanategemea Kituo cha Mbagala Rangitatu, Maji Matitu, Round table na kusababisha msongamano wa wazazi wanaohiyaji kujifungua kupungua katika hospitali ya Temeke.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo