Sharifa Marira
Tundu Lissu |
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(Chadema), ameitwa kituo cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuhojiwa
kuhusu mkutano wake na waandishi wa habari wiki iliyopita kuhusu kupotea kwa Msaidizi
wa Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, Ben Saanane.
Akizungumza na JAMBOLEO jana baada ya
kuwepo taarifa za kukamatwa kwake, Lissu alisema: “’Sijakamatwa ila nimeitwa
leo saa 2 asubuhi lakini nimefika hapa Polisi saa 4 asubuhi nimekaa hadi muda
huu saa 10.15, nimehojiwa mambo mawili.’’
Alisema amehojiwa kuhusu kauli aliyoitoa
kwenye mkutano na waandishi wa habari wiki iliyopita akituhumiwa uchochezi
kutokana na kauli kwamba kuna watu waliokamatwa sehemu mbalimbali na kuletwa
Dar es Salaam na kufungiwa Mikocheni na kuteswa.
Alisema jambo la pili ni kuhojiwa kama
shahidi kama ana taarifa zozote kuhusu kupotea kwa Saanane na baada ya
mahojiano walimwacha wakimweleza kuwa endapo wakimwitaji watamwita.
Awali kwenye mkutano wake na waandishi
wa habari, Lissu alisema Chadema haijui aliko Saanane na kuiomba Serikali
ieleze mahali alipo kwani ina jukumu la kulinda raia.
"Chadema haijui aliko Saanane,
haonekani kokote, katika mazingira haya ni vema Serikali ikaeleza kama vyombo
vya ulinzi vinamshikilia na kama havijamkamata, Mamlaka husika za mawasiliano
zieleze mara ya mwisho alifanya mawasiliano lini, wapi na nani maana ndio wenye
uwezo wa kuamuru mashirika ya mawasiliano kusema,” alisema Lissu.
Alisema wiki mbili kabla ya Saanane
kupotea kutokana aliandika katika mitandao ya kijamii akihoji uhalali wa shahada
ya tatu ya Rais John Magufuli, ambapo alipokea vitisho.
Alisema hatua hiyo ilikuja baada ya Rais
kuanzisha mchakato wa uhakiki wa vyeti kwa watumishi ambapo yeye aliliendeleza
kwenye mitandao ya kijamii.
0 comments:
Post a Comment