Abraham Ntambara
MTENDAJI Mkuu wa Mradi
wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART),
Leonard Lwakatare ameshindwa kujua ni lini wataongeza kadi nyingine za
kielekroniki kwa ajili ya abiria wa mabasi yaendayo kasi, ambazo zitaondoa kero
ya chenji na foleni wakati wa kukata tiketi.
Akizungumza na JAMBO LEO jana Dar es Salaam Lwakatare
alisema kama Serikali inawajibika kutatua kero hizo kwa kuhakikisha tiketi zinapatikana
na kubainisha kwamba mchakato unafanyika kupitia mfumo wa Sheria ya Manunuzi ya
Umma.
“Mfumo wa Manunuzi ya Umma siyo wa haraka, unahitaji
kufuata utaratibu, sasa naogopa kusema ni lini suala hili litakamilaka kwa
sababu ni mchakato, lakini tupo kwenye utaratibu wa kupata hizo kadi,” alisema Lwakatare.
Aidha alisema wamepiga hatua zaidi katika kuhakikisha wanalimaliza
suala hilo. Alibainisha kuwa, mategemeo yao ni kwamba zikipatikana tu wataanza
kuziuza kwa abiria ili zitumike.
Lwakatare aliongeza kuwa tayari walishaitisha tenda ya
kupata mtu ambaye atalishughulikia suala hilo na kusisitiza kuwa mchakato huo
uko katika hatua nzuri.
Alibainisha kama michakato yote ingekuwa imekamilika kwa
kuingia mikataba na kila kitu kuwa sawa ndiyo angeweza kujua na kusema lini
kadi hizo zitakuwa tayari kwa matumizi.
Mtendaji huyo alisema katika kuhakikisha wanasaidia kutatua
changamoto ya chenji kwa dharula wao pia wanafanya juhudi kuhakikisha chenji
zinapatikana kwenye vituo vya mabasi yaendayo kasi.
Alisema juhudi hizo zinafanyika kwa kwenda kuomba chenji hizo
kwenye benki ili kuhakikisha kuna kuwa na chenji za kutosha na kuzisambaza
kwenye vituo vyote.
Lwakatare alisisitiza kuwa ni haki ya kila mtu kupata
chenji yake bila kubaguliwa, hata kwa yule anayekuja na sh. 10000 ambapo
alibainisha kuwa ni kazi ya muuza tiketi kurudisha chenji.
Alisesitiza kuwa ni wajibu wa mtu anayeuza tiketi
kuhakikisha anakuwa na chenji za kutosha ili kuwarudishia abiria bila kuwabagua
ilimladi mtu anahitaji chenji yake.
0 comments:
Post a Comment