Mwandishi Wetu
Jaffar Sabodo |
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Jaffar Sabodo, amemshauri Rais John
Magufuli kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, akisema hali hiyo itamsaidia
kuleta tija zaidi katika utendaji wake.
Aidha, Sabodo amemshauri Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupunguza idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama
hicho pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na JAMBO LEO nyumbani kwake
Dar es Salaam, Sabodo alisema hatua hiyo itasaidia Serikali kutekeleza falsafa
yake ya kubana matumizi.
“Kupungua kwa ukubwa wa Baraza la Mawaziri kutajenga uwajibikaji
zaidi kwa mawaziri, lakini pia kubana matumizi ya Serikali kuhudumia baraza
kubwa la mawaziri pia kusaidia kujenga mfumo imara zaidi wa utawala na itakuwa
rahisi kudhibiti siri za Serikali,” alisema Sabodo na kuongeza:
“Hata ukubwa wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu za CCM nao ukipungua
utaiimarisha zaidi CCM, kwani viongozi wake watakuwa na nguvu zaidi, lakini pia
matumizi yatapungua na mambo ya chama hayatavujishwa kirahisi.”
Alipoulizwa kuhusu idadi anayopendekeza iwe kwa vyombo hivyo,
Sabodo ambaye amewahi kuwa mfadhili wa CCM na Chadema kwa nyakati tofauti
alisema: “Ili kulinda zaidi maadili ya CCM yawe kama alivyoacha Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere aliyeiasisi, kwa mawazo yangu Halmashauri Kuu ingekuwa na
wajumbe wasiozidi 55 na Kamati Kuu wawepo wajumbe wasiozidi 15.”
Kuhusu Baraza la Mawaziri Sabodo alisema linapaswa kupungua kutoka
idadi ya sasa hadi kufikia mawaziri wasiozidi 15. “Cabinet’ baraza liwe dogo,
kuna wizara zinaweza kufutwa, ili kuleta tija zaidi. Hili linawezekana,” alisema
Sabodo.
Ushauri huo wa Sabodo umekuja wakati hivi karibuni CCM ilitangaza
mabadiliko na kupunguza idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka 388
hadi 158 huku wajumbe wa Kamati Kuu ikipunguzwa kutoka 34 hadi 24.
Kwa upande wa mawaziri, Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli lina
mawaziri kamili 20 pamoja na Waziri Mkuu, likiwa na naibu mawaziri 16.
Akizungumzia uamuzi wa Rais Magufuli kuhamia Dodoma, Sabodo
alisema ameonesha uthubutu ulioshindikana kwa zaidi ya miaka 45.
Alisema anakumbuka uamuzi wa kuhamia Dodoma ulifikiwa na Bunge
enzi za utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyeshindwa kuufanikisha
kutokana na sababu mbalimbali za msingi, lakini waliofuata katika uongozi hakuna
aliyeonyesha uthubutu kama wa Rais magufuli.
Sabodo alisema hatua hiyo ya kuhamia Dodoma ikifanikiwa inaweza
kusaidia hata rushwa na ubadhirifu kupungua kwani baadhi ya mambo
yatashindikana kufanyika Dar es Salaam litakalobaki kama jiji la kibiashara
hivyo kuwalazimu wahusika kwenda makao makuu ya Serikali.
0 comments:
Post a Comment