Abraham Ntambara
WANASIASA na wasomi, wameunga mkono ushauri wa
mfanyabiashara maarufu nchini, Jaffar Sabodo kumtaka Rais John Magufuli
kupunguza Baraza la Mawaziri, lakini wamesema ni vizuri suala la idadi ya mawaziri
likawekwa kwenye Katiba ili liwe mwongozo kwa kila kiongozi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO jana
walisema ushauri huo ni mzuri, lakini inatakiwa kuwekwa kikatiba ili kumdhibiti
Rais anayetaka kuunda baraza hilo kulingana na maono yake.
Profesa Mwesigwa Baregu alikiri kuwa ushauri huo ni mzuri
na kubainisha kuwa mwisho wa siku, hilo linabaki kuwa suala la Kikatiba.
Alibainisha kuwa Katiba ina uwezo wa kusema kwamba baraza
la mawaziri lisizidi idadi fulani ya mawaziri
kwa kila Rais atakayeingia madarakani.
Hilo linatakiwa kuwa sharti la Kikatiba kama Rasimu ya
Katiba ya Warioba ilivyokuwa imependekeza kwamba Baraza lisizidi kiasi Fulani, alisema.
“Nadhani hiyo ndiyo inaweza ikasaidia kwa maana kwamba
akija Rais na akataka kulipanua Baraza, hawezi kufanya hivyo kwa sababu Katiba
inamdhibiti,” alisema Baregu.
Alisisitiza kuwa ukubwa wa Baraza la Mawaziri unatakiwa
kuwa katika Katiba. inatakiwa iwe imeainishwa kama ilivyofanya Rasimu ya Katiba ya Warioba.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa wa NCCR- Mageuzi,
Samwel Ruhuza alisema Marekani ina wananchi zaidi ya milioni 250 wakati Baraza
lao la mawaziri linaundwa na mawaziri wasiozidi 15.
Aidha aliongeza kuwa Uingereza nayo ina idadi ya watu
takribani 150, lakini baraza lao la Mawaziri linaundwa na mawaziri 20.
“Hii maana yake ni kwamba hayo yote yapo kwenye Katiba,
sasa uwingi wa mawaziri haina maana kwamba ndiyo kuna kuwa na ufanisi wa kazi,”
alisema Ruhuza.
Alibainisha kwamba baraza linapokuwa dogo inakuwa rahisi
katika kulisimamia. Alisema Katiba
tuliyonayo haimdhibiti Rais, hivyo inampa uhuru wa kuamua ukubwa wa baraza
kulingana na yeye anavyotaka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda
alisema falsafa ya kubana matumizi kwa kuwa na baraza dogo la mawaziri imekuwa
ikitumika sana hasa kwenye nchi zinazoendelea ikiwamo Marekani.
“Sasa kule Marekani hizo wizara zipo kisheria kabisa, lakini
ni chache tu wala siyo nyingi nafikiri falsafa hiyo tunaweza kuitumia,” alisema
Mbunda.
Aidha alisema kuwa cha msingi zaidi ni kuangalia kiwango
chetu ambapo tunahitaji watu wa kusukuma maendeleo katika sehemu mbalimbali na
kuongeza kwamba wakati mwingine si vyema kuwa na waziri mmoja kwenye wizara
ambayo ni kubwa kama ya Kilimo na mifugo
kwani anaweza kushindwa kuzisimamia kiukamilifu.
0 comments:
Post a Comment