Sharifa Marira na Peter Akaro
Marehemu Mpoki Bukuku |
ALIKUWA
mwandishi wa habari wa aina yake. Ndivyo unavyoweza kueleza kutokana na jinsi
watu wa kada mbalimbali, wakiwemo viongozi walivyomzungumzia Mpigapicha wa
magazeti ya The Guardian Ltd, Mpoki Bukuku aliyefariki dunia Ijumaa.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe waliongoza mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakiwemo
waandishi wa habari kuaga mwili wa marehemu huyo katika viwanja vya shule ya
sekondari Tabata Wazazi, huku wakisema tasnia ya habari imepata pigo kwa
kumpoteza mwanahabari aliyemudu kufanya kazi bila uoga, licha ya kukumbana na
vikwazo mbalimbali.
Bukuku
alifariki saa chache baada ya kugongwa na gari jirani na kituo cha mabasi cha
ITV Mwenge, wilayani Kinondoni, wakati akitoka kazini kuelekea nyumbani kwake
Tabata Kimanga.
Mwili
wa Bukuku ulisafirishwa jana kuelekea Dodoma ambako utazikwa leo.
“Tasnia
ya habari imepoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa kwa taifa kupitia
taaluma ya habari. Waandishi wa habari tumepoteza mtu muhimu kilichobaki sasa
ni kupitia kazi zake na kujifunza mazuri yote aliyoyafanya wakati wa uhai
wake,” alisema Nape.
Alibainisha
kuwa umati wa wanahabari uliohudhuria kumuaga Bukuku ni ishara kwamba wakati wa
uhai wake alifanya kazi zake kwa weledi mkubwa.
Kwa
upande wake Mbowe alisema Taifa limempoteza mtu ambaye alikuwa mstari wa mbele
kuandika habari zenye kujenga nchi.
“Katika
kumuenzi marehemu, waandishi wa habari wanatakiwa kufanya kazi bila ya woga kwa
kukosoa kwa lengo la kujenga taifa,” alisema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni.
“Simamieni
ukweli katika kuandika habari na msiogope wala kutishwa kwa sababu wananchi
wanawategemea nyinyi kupaza sauti zao.”
Mkurugenzi
Mtendaji wa The Guardian Ltd, Richard Mgamba alisema kampuni imepata
pigo kutokana uchapakazi na ucheshi na akaiomba familia kuvumilia katika
kipindi hiki kigumu
“Mpoki
alipoacha kazi Mwananchi (gazeti linalochapishwa na Kampuni na Mwananchi
Communication Ltd) baada kama ya miezi miwili alinipigia simu na kuniambia kuwa
hana kazi. Kutokana na kutambua uwezo wake nilimwambia aje na kumweleza kuwa
hastahili hata kufanyiwa usaili,” alisema Mgamba.
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat), Said Kubenea alieleza
jinsi anavyomkumbuka marehemu, huku akikumbushia tukio la Bukuku kupigwa na
askari magereza eneo la Ukonga wakati wakifuatilia baadhi ya askari hao
waliovamia nyumba za wafanyakazi wa lililokuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATC).
“Kwa
namna alivyochaniwa nguo na kulowa damu siku ile inaonyesha alikuwa anafanya
kazi kwa maslahi ya umma bila ya woga,” alisema.
“Kifo
cha Bukuku ni pigo kwa tasnia ya habari. Wakati wanahabari wakiomboleza kifo
wakuu wa wilaya wamekuwa wakiwanyanyasa waandishi wa habari,” alisema Deodatus
Balile, Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
“Tunawaonya
wakuu wa wilaya wanaowaweka mababusu na kuwapigisha magoti wanahabari waache
kwa kuwa lengo la wanahabari ni kusema ukweli daima bila kupendelea,” alisema.
Naye,
Msemaji wa familia,Alfred Mwakapesya alisema Bukuku aliyezaliwa Machi 15, 1972
ameacha mke na watoto watatu.
Alishukuru
jamii ya wanahabari, madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa msaada
wao katika kipindi hicho kigumu.
0 comments:
Post a Comment