Mwandishi Wetu
BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata),
linalosimamia sanaa na burudani nchini, limeonya wamiliki na waendeshaji wa
kumbi za burudani, kuepuka kuruhusu disko toto na kujaza watu kwenye kumbi hizo.
Aidha, Baraza hilo pia limesisitiza kuwa
halitafumbia macho ukumbi utakaokiuka maelekezo yake, ikiwa ni pamoja na
kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu hasa yanayoonesha maungo ya
ndani, kwa kuwa yameshapigwa marufuku.
Hayo yamo kwenye taarifa ya Katibu
Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari,
kwa lengo la kuwatakia wasanii na wadau
wote wa sanaa heri ya Krismasi na Mwaka mpya.
Huku ikisisitiza kauli mbihu yake kuwa
‘Sanaa ni kazi tuikuze, tuilinde na kuithamini’, Basata iliwataka wamiliki na
waendeshaji wa kumbi za burudani, kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizo
kwenye vibali vyao vya uendeshaji kumbi.
“Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na
vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa matumizi wa
kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalumu hasa makazi ya watu na
kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao,” ilieleza taarifa
hiyo.
Basata pia iliwakumbusha wamiliki wa
kumbi za sherehe na burudani, kuwa inakatazwa kukusanya watoto kwenye kumbi hizo
kupitia ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, ili
kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
“Uzoefu unaonesha, kwamba nyakati za
sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi hujisahau na kuandaa madisko toto hali
mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni
na taratibu.
“Aidha, baadhi ya wamiliki na
waendeshaji kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida bila kujali
maelekezo ya vibali vyao, wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja
waliyopangiwa na Basata,” ilieleza taarifa hiyo na kuonya kuwa hatua kali na za
kisheria zitachukuliwa kwa atakayekiuka maagizo hayo.
0 comments:
Post a Comment