Mwandishi Wetu
Edward Lowassa |
ALIYEWAHI kuwa Waziri Mkuu katika
Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa, ametumia salamu zake za Sikukuu ya Maulid
kuishauri Serikali ya Awamu ya Tano kusheherekea siku hiyo kwa kufuata mafundisho
ya Mtume Muhammad (SAW).
Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu kati
ya mwaka 2005 hadi 2008, mwaka jana alihama CCM na kujiunga na Chadema ambako
aligombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita. Alisema kama mtu anaishi katika
mafundisho ya Mtume, lazima ajifunze kuheshimiana, kuvumiliana na kupendana.
“Ninawatakia Waislamu wote nchini
kuadhimisha siku hii ya kuzaliwa kwa kiongozi wao Mtume Muhammad SAW. Waislamu
kama walivyo Watanzania wa dini nyingine wamekuwa nguzo muhimu katika kujenga
amani, upendo na utulivu nchini kwetu, na hii yote ni kutokana na mafundisho ya
kiongozi wao huyo,” alisema na kuongeza:
“Ni rai yangu kwa Watanzania wote
wakiwemo watawala kuwa tunaposherehekea siku hii tutimize kwa vitendo
mafundisho ya Bwana Mtume ambaye ni mmoja wa mitume ya mwenyezi-Mungu kwa
kuheshimiana, kuvumiliana na kupendana.”
Tangu alipojiunga upinzani, Lowassa
amekuwa akikumbana na misukosuko mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa
mikutano wa vyama vya siasa sambamba na kukamatwa kwa viongozi wa vyama hivyo
kutokana na sababu mbalimbali.
Hii si mara ya kwanza kwa Lowassa kutoa
maoni kuhusu Serikali iliyopo madarakani. Aprili mwaka huu, ikiwa ni siku 155
baada ya Rais John Magufuli kuapishwa kuwa Rais, Lowassa alitaja mambo matano
yanayomfanya autilie shaka mustakabali wa taifa chini ya uongozi wa Rais huyo
wa Awamu ya Tano.
Lowassa ambaye alishika nafasi ya pili
katika uchaguzi mkuu baada ya kupata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97
aliyataja mambo hayo kuwa ni Rais kugawa fedha wakati chombo cha kufanya hivyo
kipo, watumishi kuachishwa kazi, upitishaji wa mizigo Bandari ya Dar es Salaam
kushuka, nchi kunyimwa misaada na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi hivi
sasa.
0 comments:
Post a Comment