Abraham Ntambara
VYAMA vya upinzani nchini vimetaja mambo makubwa manne ambayo
havitayasahau mwaka huu unaoelekea mwisho wakisema yalikuwa kikwazo na mwiba
kwa upande wao.
Wapinzani hao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
walimtaja Rais John Magufuli kuwa mhusika wa wao kukumbwa na hali hiyo kwa kuidhinisha
mambo hayo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO viongozi wa Chadema,
NCCR- Mageuzi na NLD, walitaja kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara, maandamano
na kutishwa na kuwekwa ndani kuwa viliwabana kisiasa licha ya kuwa ni haki yao
kikatiba.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema jambo ambalo
hawatalisahau na lililowashitua ni kauli ya Rais Magufuli kupiga marufuku
shughuli za kisiasa za kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.
“Sasa ni sawa na mpishi, unamwambia ni marufuku kupika wakati hiyo
ndiyo haki yake, sisi siasa ndiyo kazi yetu, anazuia kazi ambazo ziko chini
yetu kihalali,” alisema Mwalimu.
Alisisitiza kuwa suala hilo liliwashitua, ni suala ambalo
watalikumbuka na kuongeza kuwa suala lingine lilikuwa ni alichokiita ubabe wa
watawala na vyombo vya Dola dhidi ya viongozi wa Chadema ambao walitishwa na
hata kupelekwa mahabusu na mahakamani.
Katibu Mkuu wa NLD, Tozi Matwange alisema jambo wasilolisahau ni
Rais kuvunja Katiba ambayo aliapa kuitumikia na kuilinda ikiruhusu vyama vya
siasa na wananchi kuwa na fursa ya kufanya maandamano, lakini aliizuia.
“Lakini Rais amevunja Katiba kuzuia vyama kufanya maandamano na
mikutano ya hadhara. Kwa kweli hilo kama chama hatutalisahau,” alisema
Matwange.
Katibu Mkuu wa NCCRMageuzi, Danda Juju alisema chama chake
hakitasahu ukandamizaji uhuru na demokrasia uliofanywa na Serikali, vitu
ambavyo vilipiganiwa tangu enzi za ukoloni ili kuwa huru kujiongoza.
“Hivi ni vitu ambavyo tumeviona katika utawala wa Rais Magufuli,
amevikalia tena sana, tunakosa uhuru na demokrasia ambavyo tulivipigania,”
alisema Juju. Alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo, inaonesha kuwapo ukiukwaji
mkubwa wa Katiba.
Naye Ofisa Habari wa ACTWazalendo, Abdalah Hamis kama vyama
vingine, alisema kwa mwaka huu, hawatasahau tukio la kuminywa kwa demokrasia na
kuvunjwa kwa Katiba kulikofanywa na Serikali.
“Kwa sababu mwaka 1992 baada vyama vingi kuruhusiwa, tuliruhusiwa
kukutana na kufanya siasa kwa ajili ya kutafuta wanachama,” alisema Hamis.
Alisema mwaka huu ulianza kwa Serikali kupiga marufuku mikutano
hiyo jambo ambalo alisema ni uvunjifu wa Katiba hivyo ACT haitasahau tukio hilo
na kuomba lisiendelee mwakani.
0 comments:
Post a Comment