*Wajumbe NEC, CC wafyekwa kuboresha utendaji
*Mpogolo, Polepole, Lubinga wapewa
majukumu
Waandishi Wetu
MKUTANO wa kwanza wa Rais John Magufuli kama
Mwenyekiti wa CCM umezaa mabadiliko 23 ndani ya chama hicho, ikiwemo kufyeka
wajumbe 230 wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), 10 wa Kamati Kuu (CC), kupunguza
idadi ya wajumbe na vikao vya ngazi mbalimbali za uamuzi za chama hicho.
Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa
jana na CCM kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye anayemaliza muda
wake kesho, chama hicho kilisema baadhi ya mabadiliko hayo yanaanza mara moja
na mengine kusubiri mabadiliko ya Katiba ya chama hicho yatakayofanyika
Februari.
Mbali na mabadiliko hayo, mkutano huo
ulimpitisha Rodrick Mpogolo kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara akichukua nafasi ya
Rajab Luhwavi ambaye ameteuliwa kuwa Balozi huku Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana
akiendelea na wadhifa huo kama ilivyo kwa wajumbe wengine watatu wa Sekretarieti.
Pia Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey
Polepole anakuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi huku Kanali Ngemela Lubinga
akiteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa,
kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk Asha Rose-Migiro.
“Halmashauri Kuu imekubaliana kupunguza
idadi ya wajumbe wa vikao vya chama katika ngazi mbalimbali ili kuongeza
ufanisi wa utendaji wa chama na kuongeza muda wa viongozi kufanya kazi za chama
kwa umma, badala ya kutumia muda mwingi vikaoni,” alisema na kuongeza:
“Ili kuwa na vikao vya chama vyenye tija,
imeamuliwa NEC sasa kuwa jumla ya wajumbe 388 ni idadi kubwa sana, hivyo
imeamuliwa idadi hii ipunguzwe na kuwa 158.”
Akichambua idadi ya wajumbe hao 158,
Nape alisema wenyeviti wa mikoa kutoka Tanzania Bara watakuwa 26 huku mikoa ya
Zanzibar wakiwa sita, wajumbe wa NEC wa mikoa watakuwa 26 kwa Bara na 24
Zanzibar, huku wajumbe wa NEC kutoka Bara wakiwa 15 na Zanzibar 15.
“Nafasi za mwenyekiti zitakuwa saba, wajumbe
wa NEC wa jumuiya watakuwa 15, wajumbe kutoka bungeni watakuwa watano, wengine
ni Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM, wajumbe watatu wa NEC kutoka Baraza la
Wawakilishi na Katibu wa Kamati ya Wawakilishi,” alisema na kuongeza kuwa
katika orodha hiyo kutakuwa na wajumbe 14 wanaoingia NEC kwa nyadhifa zao.
Pia katika mabadiliko hayo, wajumbe wa CC
walipunguzwa kutoka 34 hadi 24 huku katika ngazi ya mikoa, wajumbe watatu wa
kamati za siasa za mikoa wakipunguzwa ambao ni Katibu wa Uchumi na Fedha na
wawili wa kuchaguliwa.
“Katika wilaya wameondolewa wajumbe
wanne wa kamati ya siasa ya wilaya, huku muundo wa wilaya wa chama hicho
ukipendekezwa kuendana na muundo wa sasa wa Serikali,” alisema Nape.
Katika ufafanuzi huo, Nape alisema
mwanachama wa CCM anatakiwa kuwa na nafasi moja ya uongozi kama ilivyoanishwa
kwenye kanuni za uchaguzi za chama hicho, sambamba na kuondolewa kwa vyeo
ambavyo haviko kikatiba.
Nape pia alisema chama hicho kitafanya
uhakiki wa wanachama wake na jumuiya utakaokwenda sambamba na utoaji kadi za elektroniki
ili kuwa na udhibiti wa usahihi wa wanachama, lengo likiwa ni kuondoa makada
hewa.
“Pia uendeshaji wa shughuli zote za
jumuiya za chama na mali zake uwe chini ya usimamizi wa CCM, kubadili mwonekano
wa bendera, nafasi za makatibu wasaidizi wa mikoa na
wilaya zitaondolewa na kazi zao zitafanywa na makatibu wa jumuiya za chama wa
mikoa na wilaya kwa utaratibu utakaopangwa,” alisema.
Kuhusu tathmini ya hali ya kisiasa na
Uchaguzi wa Zanzibar ambapo NEC iliagiza kuundwa kwa kamati maalumu ya kufanya
tathimini ya kina kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar.
“Mwenyekiti wa Kamati ya Udhibiti na Nidhamu
ametakiwa akamilishe kazi ya taarifa ya udhibiti kwa wanachama waliokiuka
mienendo ya uanachama kabla ya kuanza uchaguzi mkuu wa chama mwakani. Mikoa na
wilaya ambao hawajatoa taarifa zao waziwasilishe kwa Kamati hiyo kabla ya
Januari 30,” alisema.
Kuhusu uhakiki wa mali, Nape alisema
unaendelea kufanyika, na ukikamilika taarifa yake itawasilishwa kwa
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa haraka iwezekanavyo.
Akizungumzia uamuzi huo wa CCM, Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. James Jesse alisema ni mzuri,
umepunguza gharama na kuwa utaleta ufanisi.
“Nadhani wanapaswa kupungua hadi 100
kwani walikuwa wengi hivyo naamini kuwa wataleta ufanisi katika chama,”
alisema.
Kaimu Katibu wa Shirikisho la Vyuo Vikuu
CCM, Daniel Zenda alisema wanaunga mkono uamuzi wa NEC na kuwa matarajio yao ni
chama kuimarika zaidi.
“Safu ndogo italeta mabadiliko katika
chama na naamini wanachama wataongezeka zaidi kupitia kundi hili dogo,”
alisema.
JAMBOLEO ilimtafuta Katibu mteule wa
Halmashauri Kuu ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga ili
kufahamu kuwa alikuwa amestaafu jeshini ambapo alisema amestaafu ila atazungumza
zaidi leo.
Imeandikwa
na Fidelis Butahe, Sharifa Marira na Suleiman Msuya
0 comments:
Post a Comment