Claudia Kayombo, Kibaha
IMANI za kishirikina zimetajwa kuwa chanzo cha kukimbiza waganga
na wauguzi wa zahanati ya Viziwaziwa, kwenye nyumba zilizojengwa eneo hilo kwa
ajili yao.
Zahanati hiyo iliyoko wilayani hapa, wafanyakazi wake wanadaiwa
kukimbia nyumba mbili, badala yake sasa wanaishi Dar es Salaam na hapa.
Hayo yalibainika hivi karibuni baada ya JAMBO LEO kuzuru eneo
hilo na kubaini changamoto hiyo kwa wananchi wa mitaa minne ya kata ya
Viziwaziwa wanaotegemea zahanati hiyo.
Diwani wa Kata hiyo, Mohamed Chamba na Ofisa Mtendaji wa
Kata ya Viziwaziwa, Said Mtindo walithibitisha madai hayo na kubainisha kuwa
hakuna ukweli wowote bali ni dhana tu.
Chamba alisema ni kweli hakuna mganga wala muuguzi
anayeishi kwenye nyumba hizo za zahanati na kwamba, hatua hiyo inawapa shida wananchi
wanaopangiwa sindano za saa au wanaougua ghafla usiku.
“Baada ya saa 9:30 alasiri hapa hakuna mganga wala
muuguzi, mtu akishikwa na homa ya ghafla anatakiwa kwenda Kwa Mathias, hulazimika
kusafiri kwa bodaboda kwa gharama ya kati ya Sh 5,000 na Sh 10,000 ambazo ni
mzigo mkubwa, hofu yangu wakati huu tunapoelekea masika, wananchi watapata
shida sana,” alisema Chamba.
Ofisa Mtendaji huyo alifafanua kuhusu madai hayo ya ushirikina
akisema hakuna ukweli wowote.
Akifafanua, alisema kuliwahi kuwa na madai kwamba aliyewahi
kuwa muuguzi kwenye zahanati hiyo alipotelewa na mjukuu wake katika mazingira ya
utata, lakini baadaye ikajulikana kuwa alitorokea kwa ndugu zake.
Alisema viongozi wa wilaya hiyo akiwamo Mbunge wa Viti Maalumu
walikutana na wafanyakazi hao wa afya na kuwashawishi waondokane na dhana hiyo,
lakini hawajaonesha nia ya kurudi.
Alisema jitihada za Serikali kushawishi wafanyakazi hao
wa afya zinaendelea na sasa inaunganisha huduma ya maji ili kumaliza changamoto
ambazo zinaweza kuwa sababu ya wao kutohamia kwenye nyumba hizo.
Mganga wa Zahanati hiyo, Adriene Oringo, alipoulizwa kuhusu
madai hayo, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa suala hilo liko ngazi za
juu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha, Amkauane
Ngilangwa, alisema hajui chochote kuhusu jambo hilo kwa kuwa amekaimu nafasi
hiyo kwa muda mfupi tu.
0 comments:
Post a Comment