FARU JOHN
*Maelezo
ya wakurugenzi yajikanganya, yashindwa kujibu maswali ya msingi
*Wao
wadai faru John alikuwa mkorofi, alizaa na watoto na wajukuu zake
Celina
Mathew
WAKATI mwaka ukienda ukingoni, sakata la
kupotea kwa faru John limegubikwa na wingu zito baada ya baadhi ya vigogo wa
Wizara ya Maliasili na Utalii kushindwa kutoa majibu sahihi zaidi ya
kujikanganya kwenye maelezo yao.
Hali hiyo imeendelea kuibua maswali bila
majibu ingawa tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameunda tume ya kuchunguza
utata wa faru John.
Wakati tume hiyo ikiendelea kuchunguza
sakata hilo, jana baadhi ya vigogo wa Wizara hiyo walizungumzia kifo cha faru
huyo huku wakishindwa kueleza alikufa lini na kwa ugonjwa gani na wapi
alipelekwa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa
Wanyamapori, Dk Nebbo Mwina na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Dk Idd
Mfunda walitoa ufafanuzi kuhusu faru John huku wakitofautiana na kushindwa
kutoa majibu sahihi.
Hali hiyo ilizusha maswali ya wadau
waliokuwa wakuifuatilia maelezo ya vigogo hao hata walipoulizwa swali la aina
moja kuhusu faru huyo majibu yao yalitofautiana.
Wakizungumza kwenye kipindi cha Tuongee
Asubuhi kinachorushwa na luninga ya Star TV wakurugenzi hao walisema wanatambua
tume iliyoundwa kuchunguza utata wa faru huyo.
Moja ya maswali waliyoulizwa ni kuhusu
sababu za faru John kuhamishwa kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo
Dk Mwina alijibu kuwa ilitokana na tabia yake ya kupiga wenzake na kuzaa na
ndugu zake.
Faru huyo badala ya kuhamishiwa kwenye
hifadhi nyingine ya Taifa alipelekwa kwa mtu binafsi (Grumeti) huku Dk Mwina
akisema alipelekwa Grumeti akazalishe faru wengine kwani huko kulikuwa na faru
jike.
Dk Mwina alisema kwa kuhamishiwa Grumeti
waliamini faru John asingefanya aliyokuwa akifanya Ngorongoro. “Angekwenda
Serengeti angesababisha athari mbaya kama za Ngorongoro; kuzaa na ndugu zake na
vurugu za kupiga wenzake."
Alifafanua kuwa Grumeti hawakulipa fedha
kwa kuwa faru John alikuwa chini ya Wizara na alikuwa hauzwi bali kilicholipwa
ni gharama za kumsafirisha na kushindwa kueleza ni kiasi gani kilitumika.
Walipoulizwa kwa nini hawakumpeleka
Serengeti ambako walimwomba, Dk Mwina alisema Grumeti ni wadau wao kwa kuwa walikuwa
wanaleta faru kutoka Uingereza, na faru dume waliyekuwa naye alikufa hivyo kumwomba
John.
Kuhusu kufa kwa faru John, Dk Mfunda alikiri
kuwa kweli alikufa na kuhusu kaburi lake alijibu hakuzikwa lakini pia hakuweza
kujibu kuhusu kiini cha kifo akisema hajui ugonjwa uliomuua.
Hata hivyo, wakati Dk Mwina akieleza
kuwa John alikufa Oktoba 10 mwaka jana, wachambuzi wengine kwenye kipindi hicho
walimkosoa kwa kumwambia kuwa alikufa Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa, wakati John akiwa
hifadhini waajiriwa tisa walikuwa walilipwa Sh 25,000 kila mmoja kumlinda kwa
siku, suala ambalo lilihojiwa sababu ya malipo wakati ni waajiriwa, Dk Mwina
alijibu kuwa ilikuiwa ni posho ya chakula.
Kuhusu pembe za John, Dk Mwina alisema
zilikatwa ili kupunguza makali yaliyokuwa yanasababisha vifo vya wenzake. Hata
hivyo, taarifa hiyo ilitofautiana na aliyopewa Waziri Mkuu kuwa pembe zake
zilikatika wakati anapigana.
"Hatuwezi kuanika hadharani vitu
vinavyochunguzwa.Tuache tume ifanye kazi yake, kisha watoe taarifa sahihi na
hata sisi tunazo taarifa, lakini hatuwezi kuzitoa zote kwa sasa," alisema.
Wakati Dk Mwina akitoa maelezo hayo, Dk Mfunda
alisema pembe hizo zina biashara, lakini haifanyiki Tanzania bali
wanaojihusisha nayo ni wafanyabishara haramu.
Pia alisema pembe za John tayari
zilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu na alishatoa maelekezo, kwamba hata baada ya kifo
cha faru huyo pembe zake zilichukuliwa na kuhifadhiwa ingawa hakumbuki ulikuwa
mwezi gani.
Kwenye maelezo ya vigogo hao, kuna
wakati walijibu kuwa hawakumbuki na hawajui chochote kuhusu John hali ambayo
ilimfanya mwongoza kipindi kuwauliza walichofuata kwenye kipindi wakati walidai
kwenda kutoa ufafanuzi na kuweka mambo hadharani.
Wachambuzi
Wachambuzi waliokuwa kwenye kipindi
hicho akiwamo mchambuzi wa siasa na uchumi, Herbert Faustine na mchambuzi wa
masuala ya kijamii, Cyprian Musiba walisema majibu ya wakurugenzi hao ni vema
Rais John Magufuli akayafanyia kazi kwani inaonekana wazi wapo wahusika wa moja
kwa moja.
Faustine alionesha kushangazwa na hatua
ya baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo kujikanganya wakati wakijibu maswali hayo
na kueleza kuwa takwimu ni mali ya Watanzania hivyo hawakupaswa kuzificha.
"Majibu yaliyotolewa na baadhi ya
watendaji hao wa wizara inabidi kuchunguzwa na Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa) kwani yanadhihirisha ukweli kuhusu faru John.
"Maliasili hakuna ‘jipu’ bali ni ‘saratani’.
Hivyo ni vema ikaondolewa, kwa kuwa wanashindwa kueleza ukweli kuhusu sakata
hilo," alisema.
Alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa ni
maumivu kwa Taifa endapo suala hilo litafumbiwa macho, huku akishauri kuwa umefika
wakati wizara hiyo ufumuliwe na wahusika wachukuliwe hatua kali.
Musiba alimshauri Waziri Mkuu kuondoa
wahusika wote kwani suala kama hilo la kupotea kwa faru liliwahi kutokea mwaka
1992 baada ya kupotea kwa faru mwingine.
"Wizara ile si ya kuchezea, inabidi
vikosi vya ulinzi na usalama viende kwenye hifadhi viachane na wananchi. Pia
wawepo maofisa wa usalama wa Taifa ili kufuatilia mambo yanavyokwenda kwenye
hifadhi na mbuga zetu za wanyama," alisema Musiba.
0 comments:
Post a Comment