Seif Mangwangi, Arusha
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha chini ya
Jaji wa Mahakama hiyo, Dk Modesta Opiyo, imetoa siku 10 kwa mawakili wa Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuwasilisha notisi ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Novemba 11.
Uamuzi huo wa Jaji Opiyo ulitokana na
maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa Lema, Shack Mfinanga
akiomba kumwongeza mteja wake muda wa
kuwasilisha notisi ya kukata rufaa hiyo.
“Baada ya kupitia kwa kina uamuzi wa
Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi ambako maombi yenu ya rufaa yalikataliwa kwa kuwa
nje ya muda, nimebani kulikuwa na siku mbili za mapumziko ambazo zilisababisha
rufaa yenu kuonekana kuwa nje ya muda, kwa kuwa Mahakama haifanyi kazi siku za
mapunziko,” alisema na kuongeza:
“Kutokana na Mahakama kuridhishwa na
sababu hizo, inawapa mawakili wa Lema siku 10 muwe mmeshawasilisha notisi ya
kukata rufaa.”
Baada ya maagizo hayo, upande wa
Serikali chini ya Mwanasheria Mwandamizi, Elizabeth Swai akisaidiwa na Adelaide
Kassela walikubalina na uamuzi huo pamoja na Mfinanga akisaidiwa na James Milya.
Awali maombi hayo namba 69
yaliwasilishwa mahakamani hapo chini ya hati ya dharura na wakili Mfinanga
chini ya kifungu 361(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Upande wa utetezi uliamua kuwasilisha
maombi ya kukata rufaa kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wanaotarajia kuukatia
rufaa uliotolewa Novemba 11 na Mahakama
ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha
iliyokuwa chini ya Hakimu Desderi Kamugisha.
Lema ambaye alikamatwa Novemba 2 mwaka
huu Dodoma, hadi sasa anashikiliwa na Gereza Kuu la Kisongo, Arusha, kutokana
na kusudio na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Kupinga Uamuzi wa Hakimu Mkazi, Desdery
Kamugisha aliyempa dhamana Lema katika kesi namba 440 na 441/2016 ya kutoa
lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
0 comments:
Post a Comment