Leonce Zimbandu
Dk Tatizo Waane |
MWENYEKITI
wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA), Dk Tatizo
Waane, amesema utafiti uliofanywa kwenye wilaya 53 nchini, umeonesha viashiria hatarishi
vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwamo kisukari, saratani na ugonjwa wa moyo.
Utafiti
ulifanyika 2012 na kuonesha viashiria vya magonjwa hayo, huku asilimia ikiwa
kwenye mabano, unene kupita kiasi (26), shinikizo la damu (26), mafuta mengi
mwilini (33.8) na kisukari (9.1).
Pia
utafiti huo ulibaini wananchi wanaovuta sigara (asilimia 25.9), pombe (asilimia
29.3) na wanaokula mboga mboga na matunda chini ya mara tano kwa siku ni
asilimia 97.2.
Waane
alisema hayo alipozungumza na gazeti hili Dar es Salaam mwishoni mwa wiki
kwenye uzinduzi wa kampeni ya mazoezi na kutoa fursa kwa wananchi kupima afya
zao bure.
Alisema katika
utoaji huduma ya kupima afya bure bado kuna changamoto ya uhaba wa dawa kwa
baadhi ya huduma, hivyo Serikali iliombwa kuendelea kushirikiana na wataalamu na
kupokea ushauri wao.
“TANCDA
tunaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya kuongeza uelewa kwa wananchi kwa
kutumia vyombo vya habari, matembezi na makongamano ili kupunguza magonjwa hayo
nchini,” alisema.
Alisema magonjwa
ya figo na moyo huigharimu Serikali kutibu wananchi wake nje ya nchi, hivyo
kinga ni bora kuliko tiba.
Waziri
wa Afya, Ummy Mwalimu alisema mkakati mkuu wa kufanya wananchi kufanya mazoezi
utasaidia nchi kuokoa fedha na maisha ya watu wake.
0 comments:
Post a Comment