WANASAYANSI wanaamini karibu kila mtu ana matatizo yasiyopungua matatu ya kiafya ambayo ama yamekuwa sugu au anayachukulia tu kama sehemu ya maisha yake kwa sababu haelewi tiba.
Badala ya kukaa na matatizo, gazeti hili linakupa nafasi
ya kueleza kero zako ili ujibiwe na watalamu mbalimbali wa afya.
Yafuatayo ni majibu ya baadhi ya wasomoja wa JAMBO LEO.
Swali: Dokta naomba unipe orodha angalau fupi ya vyakula
hatari kwa afya ya binadamu
Jibu: Vyakula vinavyoweza kuleta madhara kwa binadamu ni
vyote ambavyo havishauriwi au vimepigwa marufuku na wadhibiti wa vyakula kama
vile TFDA.
Ninashauri ujifunze jinsi ya kula vyakula vyenye
virutubisho sahihi (balanced diet), ambavyo ni wanga, mafuta, protini, madini,
vitamini na maji. Vyakula hivi vyote lazima vitumiwe katika kiwango
kinachohitajika.
Lakini pia tafiti zinataja baadhi ya vyakula ambavyo
vikitumi wa bila uangalifu vinaweza
kuleta madhara katika mwili wa binadamu. Baadhi ya vyakula hivi ni:
• Vyakula vyenye mafuta mengi
• Vyakula vya kukaanga mafano chips)
• Vyakula vyenye chumvi au sukari nyingi.
vile kisukari, kansa, shinikizo la damu na uzito wa
kupindukia
Ni vizuri pia kumtembelea mtaalamu wa mambo ya vyakula
(Nutritionist) kwa msaada zaidi, na pia usikose kusoma makala zijazo katika
gazeti hili ili kupata maelezo zaidi.
Swali: Nimetumia dawa za phenobabiton kwa muda wa miaka
30. Je zinaweza kuniathiri kiafya?
Jibu: Pole sana kwa tatizo ulilonalo. Swali lako
halikueleza kwa nini unatumia dawa aina ya Phenobarbital, lakini dawa hii
yaweza kutumika aidha kwa muda mfupi au muda mrefu kulingana na aina ya tatizo
ulilo nalo. Kama zilivyo dawa nyingine, Phenobarital pia ina madhara yake
inapotumika bila maelekezo maalum ya daktari. Ninakushauri urudi kwa daktari
aliyekuandikia dawa hii, au daktari mwingine yeyote mwenye uelewa wa tatizo
lako, ili muweze kuona kama bado unaihitaji au hapana, na kama dalili zote
zilizokufanya uanze kutumia dawa hii zimekwisha au bado zipo. Kiujumla dawa hii
ina madhara ya aina mbili, madhara ya muda mfupi au yale ya muda mrefu. Madhara
ya muda mfupi ni:
• Kizunguzungu, kujisikia kusinzia kila wakati, maumivu
ya kichwa, uchovu, kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika.
Madhara ya muda mrefu mengi ni yale yanayohusiana na
mfumo wa fahamu kama:
• Mabadiliko ya tabia (mfano kuwa na hasira za haraka) na
msomgo wa mawazo.
Matatizo mengine yanayoweza kutokea ni madhara ya ngozi,
madhara ya mfumo wa damu, na mifumo mingi ya mwilini.
Pamoja na madhara niliyoyataja hapo juu, ikumbukwe kuwa
si kila mgonjwa anayetumia dawa hizi ni lazima apate madhara haya. Dawa hii ni
kama dawa nyingine na inapotumika kwa nia iliyokusudiwa husaidia kutibu tatizo
kusudiwa.
Swali: Naitwa Albert. Naomba kuuliza endapo mtu utokunywa
chai je,unaweza kupata tatizo gani?
Jibu: Ndugu Albert, kama nimelielewa vizuri swali lako vizuri,
kutokunywa chai hakuwezi kukusababishia tatizo lolote. Unaweza kutafuta mbadala
kwa kunywa viburudisho vingine zaidi ya chai kama juisi, maji, maziwa na
vinginenyo.
Swali: Naitwa Justin nipo Kagera, swali langu ni kwamba
mgonjwa akiwa anafanyiwa operesheni huwa anaumia sana na je ni mbinu gani
mnatumia kuziba ngozi iliyopasuliwa?
Jibu: Ndugu Justin, hongera sana kwa kuwa na ndoto ya
kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya watoto (Paediatrician), jitahidi kusoma sana
na ndoto zako zitatimia siku moja. Mgonjwa anapofanyiwa upasuaji huwa haumii
kwa sababu hupewa dawa za kuzuia maumivu au hata za kumfanya alale usingizi
kama anafanyiwa upasuaji mkubwa.
Njia inayotumika kuziba ngozi iliyofanyiwa upasuaji ni
kwa kuishona kwa aina fulani ya nyuzi (surigal sutures) au kwa kutumia pini
maalum (staples) na kusubiri jeraha lipone kwa wakati.
Swali: Mimi ni mjamzito, nina mimba ya miezi minne lakini
nasumbuliwa na typhoid (Homa ya matumbo).
Nimetumia dawa nyingi lakini hali bado. Sasa nataka
kujaribu matibabu kwa mtu mmoja anayetibu kwa miti shamba. Je haitaleta
madhara?
Jibu: Pole sana mama. Sijajua ni dalili gani ulizonazo na
ni kipimo gani umetumia kupima tatizo lako. Ni vizuri kuwa mwangalifu kwa
sababu baadhi ya vipimo vya ugonjwa wa homa ya matumbo (typhoid fever) vinaweza
kuonesha kwamba una tatizo hilo hata baada ya miezi kadhaa baada ya kutibiwa.
Wakati wa ujauzito tunashauri dawa yoyote unayokunywa ni
lazima iwe imeshauriwa na mtaalamu wa afya ili isilete madhara katika ujauzito
wako.
Kwa kifupi baadhi ya dalili za ugonjwa wa typhoid ni joto
la mwili kuongezeka kadiri siku zinavyokwenda, maumivu ya kichwa, maumivu ya
tumbo, kuharisha au kufunga choo, kutoka jasho jingi, kukosa hamu ya kula na
tumbo kujaa gesi.
Hivyo basi, kabla ya kufanya maamuzi yoyote yale, ambayo
yanaweza kuhatarisha afya yako na ya mwanao anayetegemea kuzaliwa hivi punde,
ni lazima kuzingatia yote niliyoeleza hapo juu.
Swali: Naomba ushauri umri ni zaidi ya miaka 50 usingizi kwangu sipati kabisa nifanye nini?
Ninaweza kukaa siku mbili sipati kabisa usingizi. Nikiingia kitandani ninakuwa
kama nasubiri kuche. Mara chache naweza kusikia kama nasinzia lakini nikifika
kitandani, usingizi unaisha. Nituumie nini ili niwe napata usingizi?
Jibu: Pole sana ndugu. Kukosa usingi ni tatizo ambalo
linahitaji uchunguzi wa kina. Daktari anatakiwa kukuona na kuchukua historia
yako kwa kirefu ili kuweza kubaini tatizo.
Endapo chanzo cha tatizo lako la kukosa usingizi
(Insomnia) hakitatatuliwa, kuna hatari ya kuendelea kukosa usingizi na hatimaye
kupata madhara mengine zaidi. Tafiti mbali mbali zinataja baadhi ya sababu
zinazoweza kusababisha ukosefu wa usingizi kuwa magonjwa kama depression,
msongo wa mawazo, mabadiliko ya mazingira na ratiba za siku, baadhi ya madawa
kama nicotine (inapatikana kwenye sigara) na caffeine (inapatikana kwenye
kahawa na chai ya rangi).
Sababu nyingine ni ulevi na baadhi ya magonjwa ya akili.
Hivyo unatakiwa kumuona mtaalamu wa afya li aweze kujua kama unahitaji kupewa
dawa au kupewa ushauri na matibabu mengine zaidi.
Swali: Naitwa Baraka, nipo Tabora nina tatizo la kukojoa
mkojo wa njano unatoka wa moto sana halafu kwa ndani kunawasha, natamani
kujikuna muda wote. Je nitumie dawa gani ili niweze kupona tatizo hilo?
Jibu: Pole sana Baraka. Kutokana na dalili ulizozitaja
inaonekana una tatizo la maambukizi ya bakteria ya njia ya mkojo au kwa lugha
ya kitaalamu ni UTI.
Dalili nyiningine za UTI ni kama kukojoa mara kwa mara,
maumivu chini ya tumbo, homa kali, kujisikia mkojo umejaa kwenye kibofu ili
hali ukienda kukojoa hupati mkojo kwa kiasi ulichotegemea.
Ninakushauri uende hospitali ya karibu ili umpe daktari
historia kamili ya matatizo yako na yeye atakufanyia vipimo sahihi vikiwemo vya
mkojo, na kukutibu tatizo lako. Pia nakushauri unywe maji kwa wingi, hii itakusaidia
kubadili rangi ya mkojo wako kuwa ya kawaida.
Swali: Mimi ni msichana wa miaka 26, tatizo langu kila siku
tumbo langu linakuwa kubwa kuzidi ujauzito wenye muda wa kujifungua. Je
nifanyeje. Maana kila nikienda hospitali kupimwa sikutwi na tatizo ambalo
linaweza kuwa chanzo cha tumbo langu kuwa kubwa. Anna,Temeke Dar es salaam.
Jibu: Pole sana Anna. Sababu za tumbo kuwa kubwa zipo
nyingi, ni vigumu kuzitaja zote katika nafasi hii ndogo. Pia ingekua rahisi
kwangu kama ningejua ulipoenda hospitali ni vipimo gani ulifanyiwa.
Ninakushauri urudi hospitali na uombe kuonana na daktari
bingwa (Physician). Kama hapatikani katika hospitali yako, basi waweza kuomba
rufaa ili uende kwenye hospitali kubwa zaidi kwa ajili ya kumuona daktari
bingwa na kufanyiwa vipimo na matibabu zaidi.
Swali: Naomba kujua tumbo la chakula kwa kawaida
linatakiwa lipate chakula chenye kipimo cha uzito gani kwa mlo?
Jibu: Kwa kawaida kiasi cha chakula unachotakiwa kula hakipimwi
kwa mzani fulani. Kinachotakiwa kufahamika ni kipimo gani cha nguvu (energy)
mtu anatakiwa apate kwa siku.
Kipimo hiki huitwa kalori (calorie), na mwanaume wa
kawaida mwenye uzito wa wastani anahitaji angalau chakula chenye kalori 2500
(2500 calories) kwa siku, wakati mwanamke mwenye uzito wa wastani anahitaji
angalau kalori 2000 (2000 calories) kwa siku.
Swali: Natamani kujua tiba ya fangas sehemu za siri. Nawashwa
ukeni. Haja ndogo naumia. Nikifanya tendo la ndoa navimba. Mara kwa mara
natokwa na uchafu ukeni. Ni uchafu mweupe na wakati mwingine una rangi ya
njano. Je sababu ni nini? Ni ugonjwa gani?
Jibu: Pole sana ndugu. Kwa dalili ulizozitaja kwenye
swali lako inaoneka una maambukizi ya fangasi aina ya candida za ukeni.
Fangasi za ukeni husababishwa na mabadiliko ya hali ya
asidi ambayo ndiyo inayotakiwa kuwepo ukeni, badala yake hali ya alikali
(Alkaline) huongezeka, hii husababisha kupungua kwa baadhi ya bakteria wenye
faida ambao ndio huzuia kusambaa kwa candida. Tatizo la fangasi za ukeni pia
hutokea mara kwa mara kwa akina mama wajawazito na wale wasio wajawazito hasa
wakati wa hedhi. Ninakushauri uende hospitali kwa vipimo na matibabu kwa sababu
tatizo hili linatibika.
Swali: Naitwa Rajab Kaila. Ni dereva. Huwa napata tabu
usiku nikiwa naendesha lori. Nasumbuliwa na usingizi sasa. Naomba ushauri nini
cha kufanya ili nisipate usingizi wakati wa usiku nikiwa naendesha.
Jibu: Ndugu Rajab, kwa kawaida inapofika usiku ubongo na
mwili kwa ujumla vinahitaji kupumzika. Ninakushauri ni vizuri ukau-tumia usiku
kupumzika kiasi cha kutosha na mchana kuendelea na safari yako.
Kama ni muhimu sana kusafiri usiku kutokana na aina ya
kazi yako, basi ninakushauri upate muda wa kutosha wa kulala nyakati za mchana.
Binadamu anahitaji angalau masaa saba mpaka nane ya kulala kila siku.
Kutokuzingatia hili, kunaweza kukupelekea kupata madhara
mengine ya kiafya na hata uwezekano wa kupata ajali barabarani.
Maoni au maswali tuma kwa simu 0713247889 au kwa
baruapepe: afya@jamboleo.net
0 comments:
Post a Comment