Jemah Makamba na Haji Kameta (Daystar)
WABUNGE wa Mikumi, Joseph Haule na Chalinze, Ridhiwan Kikwete wamelaani
kitendo kilichofanywa na jamii ya wafugaji kwa kujichukulia sheria mkononi na
kumjeruhi kwa mkuki mkulima Augustine Mtitu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, kuhusu tukio hilo lilitokea
katika kijiji cha Upangwani, Masanze, Mikumi, wabunge hao waliezea kusikitishwa
kwao na kutaka hatua zichukuliwe.
“Ni kitendo cha kusikitisha sana kwa hawa ndugu zetu wafugaji walijiamulia
kufanya kitendo cha kinyama kama hiki, huu si ubinadamu kabisa,” alisema Haule.
Alisema mkulima huyo alichomwa mkuki na wafugaji wa Kimasai
alipokuwa akimsaidia jirani yake kufukuza ng’ombe wasiharibu mazao shambani mwake.
Alisema Mwenyekiti wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji nao
walijeruhiwa na wafugaji hao. “Sisi Ofisi ya Mbunge wa Mikumi tunatoa mwito kwa
Serikali kubaini waliofanya vitendo hivyo na kuwakamata ili kuvikomesha,” alisema
Haule.
Alisema atashirikiana na Serikali kukomesha migogoro isiyokwisha
kati ya wakulima na wafugaji Kilosa.
Ridhiwan naye alilaani vitendo hivyo na kuishauri Serikali
kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo hilo.
“Ni lazima Serikali ije na majibu sahihi, ili kunusuru vita vya
wenyewe kwa wenyewe visitokee kati ya jamii hizo. Si ajabu kusikia mtu kavunjwa
mgongo, mwingine mlemavu, leo kapigwa mkuki wa midomo ukatokea shingoni, kilio
hiki kipo katika masikio ya watu wengi kuhusu mapigano ya wakulima na
wafugaji,” alisema.
Aliongeza: “Serikali isikie hili na kuchukua hatua stahiki ya kudhibiti
kabla damu ya Watanzania wanyonge wanaotegemea kilimo kama kiinua mgongo chao
hawajapotea. Kuna sheria na mipango ya matumizi bora ya ardhi, zitumike.”
Ridhiwan alisema jambo la msingi ambalo Serikali inatakiwa kujua
ni kwamba hali ilivyo sasa, si ya kufanyia mzaha na waziri husika ayafanyie
kazi.
Alisema binafsi analaani vitendo hivyo na kuiasa Serikali
kujipanga vizuri kabla mambo hayajaharibika. “Yalianza Kilosa, Mvomero, Chalinze,
Handeni, Kiteto na sasa Mikumi. Serikali jipangeni, kabla hapajachafuka,”
alihadharisha.
0 comments:
Post a Comment