Charles James
John Guninita |
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa
Dar es Salaam, ambaye sasa yuko Chadema, John Guninita, amekataa kumsamehe
aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye.
Guninita alifikia hatua hiyo jana alipoulizwa
na mwandishi wa habari hizi, kueleza msimamo wake baada ya Nape kuomba msamaha
kwa wanasiasa na viongozi wa vyama vya Upinzani kwa kauli zake alizopata
kuzitoa, huku akimtuhumu Waziri huyo wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo kuwa ni mnafiki.
Tofauti na msimamo wa Guninita, kada
mwingine wa zamani wa CCM, Khamis Mgeja ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani
Shinyanga, naye sasa kuwa Chadema, alisema kilichofanywa na Nape ni kitendo cha
kiungwana.
Nape aliomba msamaha huo wakati
akimkabidhi ofisi, mrithi wake, Humphrey Polepole, aliyeteuliwa na NEC kushika
nafasi hiyo katika mabadiliko ya ndani ya chama yaliyofanywa mapema wiki hii.
Guninita alisisitiza kuwa msamaha ulioombwa
na Nape kwa wapinzani ni wa kinafiki, kwa sababu alitoa kauli hizo akiwa kwenye
majukumu ya chama chake, hivyo msamaha huo alipaswa kuomba wanachama wenzake
ndani ya CCM.
Alisema Nape alikuwa na haki ya kuomba
radhi wanasiasa ndani ya chama chake, kwa sababu ndio anaendelea kushirikiana
nao katika majukumu ya chama chao, huku akisema ataendelea kupambana na
wapinzani kwenye majukwaa ya kisiasa, hivyo msamaha huo ni sawa na bure, kwani
bado ataendelea kukumbana nao kutokana na kuwa na misimamo tofauti kiitikadi.
“Unajua, kwenye siasa mtu unapotoa
matamko yoyote hasa ukiwa kwenye nafasi kama aliyokuwa nayo yeye, ujue uko
kazini na unafanya kazi uliyotumwa na chama, hivyo kuomba msamaha ni sawa na
kuonesha unafiki kisiasa,” alisema Guninita.
Akizungumzia kauli zilizowahi kumkera na
kuumiza wapinzani kuwa ni pamoja na ile ya ‘goli la mkono’, ‘wapinzani ni
majitaka’, na ya kuwaita waliojitoa CCM kwenda Upinzani kuwa ‘makapi’ huku
akisema zilikosa busara na uungwana.
Mgeja
Hata hivyo, Mgeja alifafanua kuwa
kilichofanywa na Nape hata kwenye vitabu vya dini imeandikwa, kuwa mtu
anapokosea, anapaswa kuomba radhi huku akisema atamkumbuka kwa kauli zake za
kuudhi wapinzani, ikiwamo aliyotoa wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana kuwa ‘CCM
itashinda hata kwa bao la mkono’.
“Nape bado ni kijana mdogo na pengine
kauli alizokuwa akitoa zilitokana na utoto na kulewa madaraka, hivyo kama
ameamua kuomba msamaha ni wazi ameonesha kukua kisiasa na anapaswa kupongezwa
na kusamehewa,” alisema Mgeja.
Wawili hao walijiondoa CCM na kujiunga
na Chadema Agosti 13 mwaka jana, baada ya walichokieleza kuwa ni kutoridhishwa
na mwenendo wa chama hicho kwenye mchakato wa kupata mgombea urais.
0 comments:
Post a Comment