Grace Gurisha
Maxence Melo |
MMILIKI
wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo, amepandishwa kizimbani mara tatu kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka manne
likiwamo la kuzuia upelelezi wa Polisi kuhusu mtandao huo.
Ilikuwa
kama sinema jana, kwani Melo alipandishwa kwa mahakimu watatu tofauti na kila
alipopata dhamana kwa hakimu mmoja, askari walimkamata na kumrudisha mahakamani
kwa hakimu mwingine na kusomewa mashitaka mengine, kabla ya kushindwa masharti kwa
hakimu wa tatu.
Baada ya
Melo kutoka kwa hakimu huyo na kurudishwa mahabusu mahakamani hapo,
alichukuliwa na gari la Polisi na kuondolewa eneo hilo, akiwa chini ya ulinzi
wa askari zaidi ya sita.
Melo
alionekana mwenye huzuni akiwa amekalishwa chini kwenye gari hilo.
Hatua
hiyo ilifikiwa na Jeshi hilo baada ya Melo kushindwa kutimiza masharti ya
dhamana katika kesi ya mwisho kati ya tatu alizoshitakiwa kwa wakati mmoja,
ambapo alitakiwa awe na wadhamini wawili wa kuaminika waliotakiwa kusaini bondi
ya Sh milioni tano kwa kila mmoja.
Mashitaka
Melo
ambaye ni Mkurugenzi wa Jamii Media Co Ltd, alipandishwa kizimbani kwa mahakimu
wakazi watatu, Mwandamizi Thomas Simba, Victoria Nongwa na Godfrey Mwapamba.
Wakili
wa Serikali, Mohamed Salum alidai mbele ya Simba kuwa katika tarehe
zisizofahamika kati ya Aprili mosi na Desemba 13, akiwa Mikocheni, Dar es
Salaam akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media na mwendeshaji wa Jamii Forums, alizuia
upelelezi.
Alidai
kuwa akiwa katika ofisi hizo akifahamu kuwa Polisi inafanya uchunguzi wa makosa
ya mtandao kupitia tovuti yake kuona kama alikiuka Sheria ya Mitandao, alikataa
kutoa taarifa za elektroniki.
Melo
akiwa mbele ya Hakimu Mwambapa, alidaiwa kuwa tarehe zisizofahamika kati Mei 10
na Desemba 13, akiwa eneo hilo, alizuia upelelezi wa Polisi kwa kukataa kutii
amri za kutoa taarifa za mtandao wake.
Katika kesi
ya tatu, Melo alipandishwa kizimbani kujibu tuhuma mbili mbele ya Hakimu Nongwa;
kuzuia uplelezi na kuendesha mtandao bila
kuusajili.
Salum
alidai kuwa siku zisizofahamika kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13 mwaka huu,
akiwa Mikocheni, aliendesha mtandao wa ‘jamiiforums.com’ bila kusajiliwa na
mtandao wa Tanzania (do-tz).
Dhamana
Baada ya
Melo kusomewa mashitaka alikana kuhusika, na upande wa Jamhuri kudai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba siku nyingine ya kutajwa kesi
hizo, huku ukidai kuwa hauna pingamizi la dhamana kwa mshitakiwa.
Mawakili
wa Melo, Jebra Kambole na Mtobesya, waliiomba Mahakama impe dhamana mteja wao
kwa sababu tuhuma zake kisheria zinadhaminika na pia ni haki yake kupata
dhamana, hivyo kuomba masharti nafuu.
Hakimu
Simba alisema ili awe nje kwa dhamana, alitakiwa awe na wadhamini wawili wa
kuaminika, kila mmoja asaini bondi ya Sh milioni 10, Melo alitimiza masharti
hayo na kuachwa kwa dhamana.
Baada ya
kuachwa, alikamatwa na kupandishwa tena kwa Hakimu Nongwa, ambaye alitaka
mshitakiwa awe na wadhamini wawili, wasaini bondi ya Sh milioni moja kila mmoja,
au ajidhamini kwa kusaini bondi hiyo.
Alipotoka
hapo, alipandishwa kwa Hakimu Mwambapa, ambaye alitaka mshitakiwa awe na
wadhamini wawili, wasaini bondi ya Sh milioni tano kila mmoja, ambapo Melo
alishindwa masharti hayo na kujikuta akirudishwa mahabusu.
Kesi
hizo ziliahirishwa hadi Desemba 29 zitakapotajwa na kuangalia kama upelelezi
umekamilika.
0 comments:
Post a Comment