Emeresiana Athanas
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
imesitisha mchakato wa uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za udiwani katika Kata
za Mkoma na Mwamtani unaotarajiwa kufanyika Januari 22 mwakani.
Akizungumza Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima, alisema kuwa hatua hiyo
imefikiwa baada ya tume hiyo kujiridhisha kuwa kata hizo haziko wazi kisheria.
"Tume imefuatilia na kujiridhisha
kuwa kata hizo ni kweli haziko wazi kwa mujibu wa sheria na hivyo kutoa maamuzi
ya kuziondoa katika orodha ya kata zilizotangazwa kufanya uteuzi wa wagombea na
kufanya uchaguzi,"alisema.
Alifafanua kuwa katika kata ya Mkoma
iliyopo Halmashauri ya Rorya mkoani Mara, diwani alishindwa kesi yake katika
mahakama ya chini na kuamua kukata rufaa mahakama ya juu, hivyo kuifanya nafasi
hiyo kutokuwa wazi kwa kuwa uamuzi unaweza kubadilika na kuendelea kuwa diwani
wa kata hiyo.
Aidha katika kata ya Mwamtani iliyoko
Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, alisema diwani wake ana sifa za kuendelea
kushikilia nafasi hiyo kwa mujibu wa sheria kutokana na kumaliza kifungo chake
cha miezi sita.
"Diwani wa kata hii alihukumiwa
kifungo cha miezi sita na tayari ametumikia kifungo hicho hivyo kwa mujibu wa
sheria bado anasifa ya kuendelea kuwa diwani wa kata hiyo," alisema.
Kata hizo ni miongoni mwa kata 22
zilizotangazwa na tume hiyo kuwa zitafanya uchaguzi mdogo kujaza nafasi wazi za
madiwani kwenye halmashauri mbalimbali Tanzania Bara.
0 comments:
Post a Comment