*Amporomoshea matusi Mhariri kwa simu ya mwandishi
*Kisa ni
swali kuhusu cheti chake cha kidato cha nne
Mwandishi
Wetu
Paul Makonda |
SWALI
aliloulizwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuhusu tuhuma
zilizosambaa mitandaoni, kwamba anatumia cheti cha kidato cha nne cha mtu,
zimeibua jambo jipya kuhusu tuhuma hizo.
Badala
ya kujibu swali hilo, Makonda jana alitoa lugha ya vitisho na matusi kwa
Mhariri wa Habari wa gazeti hili, Exuperius Kachenje, akitumia simu ya mwandishi
aliyemuuliza swali hilo, Salha Mohammed.
Awali
gazeti hili lilianza kufuatilia madai ya Makonda kukosa cheti cha kidato cha
nne, kutokana na hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Tano, imeshazichukua dhidi
ya watumishi wa umma, wasiokuwa na vyeti hivyo ambao walishafukuzwa kazi na
wako hatarini kupoteza mafao yao.
Ufuatiliaji
Katika jitihada
kusaka ukweli kuhusu madai hayo, gazeti hili tangu wiki iliyopita lilizungumza
na anayedaiwa kumpa cheti hicho Makonda, aliyejitambulisha kwa jina la Paul
Pierre Christian.
Gazeti hili pia lilipata taarifa za ziada kutoka katika
chanzo chake, zilizoeleza madai ya ukaribu wa Makonda na Christian katika
maisha ya ujana wao.
Jitihada ziliendelea kutafuta taarifa sahihi, ambapo
gazeti lilikuwa katika mchakato wa kupata taarifa kutoka shule ya msingi
Kilomije, iliyopo wilayani Kwimba, kujua jina sahihi la kwanza alilotumia
Makonda alipokuwa akisoma shuleni hapo, ambalo inadaiwa si Paul.
Kabla ya kukamilika kwa mchakato huo, ndipo gazeti lilipopata
taarifa za kuwepo kwa mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Mkuu huyo
wa Mkoa, kuhusu kupatikana kwa
eneo la kujenga viwanda vidogo jijini humo, iliyochapishwa ukurasa wa nane wa
gazeti hili.
Kutokana na umuhimu wa taarifa hizo, Kachenje alimwelekeza Salha, kutumia fursa hiyo
kihabari kuzungumza pembeni na kiongozi huyo, ambapo katika hali ambayo
haikutarajiwa, Makonda aliagiza simu ipigwe kwa mhariri na kutoa kauli ambazo
hazikutarajiwa.
Makonda
Makonda
alimuagiza Salha, kumpigia simu mtu aliyemtuma kuuliza swali hilo, ambaye ni
Kachenje ili ampe jibu mtu huyo badala ya mwandishi.
Kupitia
simu hiyo iliyopigwa saa 5:45 ambapo rekodi zinaonesha mazungumzo ya awali
yalichukua sekunde 30, kisha akapiga tena saa 5:46 na kutumia sekunde 13, Makonda
alihoji iwapo swali lililoulizwa kwake litasaidia kumtoa, Mshauri wa Kampuni za
Quality Group, Yusuf Manji katika kesi inayomkabili kuhusu matumizi ya dawa za
kulevya.
Aidha,
Makonda alitumia simu hiyo ilipopigwa kwa mara ya pili, kumtisha mhariri huyo
kwamba asisikie amemtisha mwandishi Salha.
Alipotakiwa
kueleza zaidi tukio hilo, Kachenje alisema simu ya Salha ilipoingia kwake,
hakuwaza jambo lolote zaidi ya kutarajia kupewa dondoo za awali za mkutano
alioitisha Makonda, kwa kuwa ndio utaratibu wa kawaida wa mwandishi, kumuarifiwa
mhariri kilijiri katika utafutaji habari.
“Nilisikia
sauti ya Salha ikisema, huyu hapa ongea naye, nikauliza ni nani, mwandishi
akajibu RC. Kusikia hivyo nikamsalimu, badala ya kujibu salamu, akanza kutoa
maneno,” alisema Kachenje.
Sehemu
ya mazungumzo hayo ya Makonda na Mhariri wa Habari wa gazeti hili kupitia simu
ya Salha ni kama ifuatavyo:
Mhariri:
“Mheshimiwa habari?”
RC Makonda:
“Unadhani majibu ya swali hili yatamtoa Manji kwenye kesi ya dawa za kulevya?”
Mhariri:
“Mheshimiwa, hilo linakujaje, sisi tunataka kujua kuhusu wewe?”
RC
Makonda: “Nasema hivi, unadhani majibu ya swali hilo (kuhusu elimu yake) yatasaidia
kumtoa Manji kwenye kesi ya dawa ya za kulevya? Huna akili wewe.” Alisema
Makonda kisha akakata simu.
Hata
hivyo, sekunde chache baadaye alipiga tena simu na Mhariri alipotaka ufafanuzi
zaidi, Makonda alisema: “Na nisikie unamtisha au kumnyanyasa huyu mwandishi (Salha),”
kisha akakata simu.
Mwandishi
alivyouliza
Akisimulia alivyomfuata Makonda ili kumuuliza swali hilo
baada ya kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari Kisarawe 11 wilayani
Kigamboni, Salha alisema alimuomba pembeni Mkuu huyo wa Mkoa ili amuulize swali
hilo.
Kwa mujibu wa Salha, Makonda hakuwa na shaka na alikubali
ombi hilo lakini baada ya kuulizwa swali hilo, Mkuu huyo wa Mkoa aliomba nafasi
ili amjibu Mhariri moja kwa moja kupitia simu yake (mwandishi) na mwandishi
huyo alitii. Mahojiano ya Salma na Makonda yalikuwa kama ifuatavyo;
Mwandishi: Shikamoo.
RC Makonda: Marahaba.
Mwandishi: Kuna taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba
unatumia cheti cha mtu cha sekondari, taarifa hizo ni kweli?
RC Makonda: Amekutuma nani?
Mwandishi: Nimetumwa na ofisi, bosi wanngu amenituma.
RC Makonda: Mpigie nimjibu.
Ndipo mwandishi akampigia Mhariri wa Habari naye alipokea
simu hiyo na kutoa majibu aliyotoa.
Akizungumza tukio hilo, Salha alisema majibu ya Makonda
yalimfanya ashangae kwa kuwa hakutegemea jibu alilosikia.
Katibu TEF
Akizungumza
kuhusu tukio, Katibu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena alisema
alichofanya Makonda kinapingana na Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016
kifungu cha 7.
“Kifungu
hicho kinaeleza majukumu ya kisheria kwa mwandishi wa habari kutafuta taarifa
na hilo linafanyika ili kuujulisha umma, pili ni suala la weledi.
“Kama
Mkuu wa Mkoa, Makonda alifuatwa na kuulizwa kuhusu taarifa kwamba hana cheti
cha kidato cha nne, ambazo zimezagaa katika mtandao, hapo alipaswa kujibu
tuhuma badala ya kumshambulia Mhariri wa Habari,” alisema Meena na kuongeza:
“Makonda
asitufikishe mahali vyombo vya habari vikaacha kutuma waandishi kwenye mikutano
yake, itafika mahali tutawazuia na lazima niseme anakwenda kubaya. Asipambane
na vyombo vya habari. Alitaja watu katika tuhuma, naye akitajwa asikilize na
kujibu hoja.”
Madai
mtandaoni
Mwishoni
mwa wiki iliyopita kulizagaa taarifa kwenye mitandao ya jamii, zikidai kwamba
Makonda anatumia cheti cha mtu cha kidato cha nne.
Taarifa hizo
zilidai kuwa jina la kwanza analotumia Makonda ni la mtu mwingine anayetajwa
kusoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Wavulana Tabora, baada ya
kufaulu vizuri kidato cha nne, na sasa ni mtangazaji katika redio moja ya jamii
mkoani Tabora.
Katika jitihada za kupata taarifa sahihi, gazeti hili
lilifanikiwa kumpata mtoa habari aliye karibu na anayedaiwa kutoa cheti cha
kidato cha nne chenye ufaulu wa daraja la kwanza kwa Makonda.
Mtoa habari huyo alimtaja anayedaiwa kuwa mmiliki wa
cheti anachotumia Makonda, kwa jina la Paul Cristian na kwamba Mkuu huyo wa
Mkoa na mtangazaji huyo, ni marafiki wa karibu na ni kama watoto waliolelewa
katika familia moja.
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, madai yaliyosambaa katika
mtandao kwamba Makonda alipata sifuri kidato cha nne si kweli, ila alitoa
taarifa zingine kutilia shaka jila la Paul, analotumia Makonda sasa.
(mazungumzo mengine yamehifadhiwa).
Anayedaiwa kumiliki cheti
Gazeti hili lilifanikiwa kumpata mwandishi anayedaiwa
kumpa cheti cha kidato cha nne Makonda, ambaye alijitambulisha kwa jina la Paul
Christian.
“Paul Makonda nimemfahamu kupitia habari, na jina
wanavyolitaja (waliotunga taarifa ya mtandaoni) wanakosea kwani mimi naitwa
Paul Pierre Christian Kagezi, hatuna uhusiano, mimi Mhaya yeye Msukuma.”
Alisema watu wanaooanisha majina pasipo kufanya utafiti wa
kutosha, wangeuliza kwanza kabla ya kutoa na kusambaza taarifa kwenye mitandao.
“Taarifa hizo (za kumpa cheti Makonda) si za kweli kwa
sababu huwezi kutoa cheti wakati umepata daraja la kwanza kidato cha sita, utakwenda
vipi chuo kikuu? Sasa niliwezaje mimi kwenda chuo kikuu halafu kwa wakati huo
nimpe naye aende chuo kikuu?”Alihoji.
Cristian aliendelea kudai kuwa katika kidato cha tano na
sita, alichukua mchepuo wa sayansi masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM),
hivyo si rahisi kutoa cheti hicho kwani angeshindwa kumudu huko alikokwenda.
Alihoji kama Makonda hakufanya vema kidato cha nne au hakusoma
kidato cha sita, akatumia cheti cha mtu mwingine, angeweza vipi kufanya vema
katika mitihani yake ya chuo kikuu?
Alifafanua kuwa watu wamekuwa wakipika na kuoanisha
majina yao, huku akiendelea kukanusha kuhusu taarifa hizo.
“Kama wanataka kumpata huyo bwanamdogo (Makonda) kwa njia
hiyo wamemkosa, kwani kwa mantiki nimekuuliza ukipata daraja la kwanza kidato
cha sita lazima uende chuo kikuu?” Alihoji baada ya kushindwa kujibu swali la
mwandishi kuhusu chuo kikuu alichosoma na ilikuwaje akawa mwandishi wa habari.
Christian aliendelea kudai kuwa kutumia cheti kimoja kwa
vyuo viwili vya Serikali, ni jambo lisilowezekana akimaanisha Makonda
asingeweza kutumia cheti alichokuwa akitumia yeye.
“Sera ya Serikali ni kwamba unapata asilimia 100 ya
mkopo, inakuwaje mtu huyo nimpe cheti changu wakati huo naye anakwenda chuo
kikuu ambacho nacho ni cha Serikali?” Aliendelea kuhoji.
“Huyo bwana anajitegemea yeye kama yeye, na
walichokifanya wao (waliosambaza taarifa mtandaoni) kwa makusudi yao bila shaka
wana lengo lao, wao wametaka kuingiza hoja ambazo hazina mashiko.
“Cheti cha daraja la kwanza unauza kwa gharama gani?
Nimesoma shule ya msingi na sekondari, (Makonda) alikuwa na fedha kiasi gani za
kunipa ili nimuachie cheti? Inaweza kukuingia akilini kweli?”Alihoji Christian.
Alidai hata namba ya Makonda hana, huku akibainisha
kutokumbuka namba za shule alikomaliza kidato cha nne pamoja na za cheti chake
cha kidato cha nne.
0 comments:
Post a Comment