Moses Ng’wat, Mbeya
BWANA harusi Samwel Mwakalobo, aliyetelekeza Bibi
harusi, Given Mgaya kanisani Ijumaa iliyopita, Desemba 16, amerejea kanisani na
mwenzake huyo na kufunga ndoa, huku akisema alipoteza ufahamu wake aliposusa
kwenda kanisani siku hiyo.
Mwakalobo na Given walikula kiapo cha uaminifu
katika ndoa yao jana saa 9.38 alasiri kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Usharika wa Isanga jijini hapa, mbele ya Mchungaji Andangile
Mwakijungu na baadaye kukabidhiwa vyeti vyao, baada ya Mwakalobo kwenda kumwomba
ndoa yao iendelee.
Mapema asubuhi mwandishi wa JAMBO LEO alipigiwa
simu na Mwakalobo akimwomba afike nyumbani kwake kwa mazungumzo, baada ya Bwana
harusi huyo kushindwa kuzungumzia suala hilo tangu siku ya tukio, wiki
iliyopita.
Alipofika, Mwakalobo alimkaribisha katika ibada ya
ndoa hiyo, ambapo alikwenda kwenye Kanisa hilo, ambapo alishuhudia Mwakalobo na
Given wakitangazwa kuwa wanandoa halali, kwa mujibu wa taratibu za KKKT na
sheria za Tanzania.
Akielezea ilivyokuwa baada ya kufunga ndoa hiyo,
Mchungaji Mwakijungu alisema alifuatwa na Mwakalobo kumwomba ampe nafasi ya
pili ya kutimiza ahadi yake ya ndoa kwa mchumba wake Given.
Akisimulia tukio hilo baada ya kuruhusiwa na
Mchungaji mbele ya mashuhuda, Mwakalobo alisema hakuwa akijitambua tangu Ijumaa
ya wiki iliyopita hadi Jumatatu wiki hii.
Alisema baada ya kujitambua, alikimbilia kwa
Mchungaji Mwakijungu kumwomba msamaha kwa yaliyotokea na kusema yalikuwa mapito
na anajuta kukosa madhabahu ya Mungu.
Akizungumza ibadani hapo, Mchungaji Mwakijungu
aliyetumia zaidi ya saa moja na nusu, alitoa wosia kwa maharusi hao na kuonya
waumini waliokuwa wakizungumza mambo yasiyo ya ukweli, kuhusu tukio hilo.
Wazazi wa pande mbili walipopewa nafasi ya
kuzungumza, walielezea namna tukio hilo lilivyowaimarisha, huku waumini
wakisema: “Huyu ndiye Mungu anayeishi.”
Given aliyekuwa na wakati mgumu wiki iliyopita,
aliwaomba msamaha waumini wote kwa niaba ya familia yake mpya na mumewe, na
kuongeza kuwa wataendelea na maisha yao.
Desemba 16, Given ambaye ni mkazi wa Chimala, Mbarali,
alikutwa na mkasa huo unaoelezwa kuwa mgumu zaidi katika maisha ya binadamu; wa
kuachwa na mumewe mtarajiwa, siku ya harusi.
Given alipata taarifa mbili muda mfupi baada ya
kutoka saluni, ambako alikuwa akipambwa tayari kwa ajili ya kwenda kanisani,
lakini haikuwa rahisi kuziamini mpaka alipokwenda kuhakikisha kanisani.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa masharti
la jina lake kuhifadhiwa, mmoja wa wapambe wa Bibi harusi alidai kuwa walipata
taarifa ya kwanza muda mfupi baada ya kutoka saluni.
Kwa mujibu wa madai ya mpambe huyo, walimpigia simu
Mwakalobo kumpa taarifa kuwa wako tayari; kwamba Bibi harusi na wapambe wake
wameshapambwa tayari kwenda kanisani.
“Tulishangazwa na Bwana harusi, kwani alitujibu kwa
mkato kuwa hawezi kuendelea na tumpeleke Bibi harusi kwa wazazi wake, akakata
simu,” alisimulia mpambe huyo.
Mshangao huo ulisababisha wampigie simu Mwakalobo
kwa mara ya pili ili kupata uhakika, ambapo mpambe huyo alidai simu ya Bwana
harusi haikupatikana.
Wakati wakiwa kwenye taharuki, mpambe huyo alidai
kuwa walipata taarifa ya pili, baada ya Mwakalobo kutuma ujumbe mfupi wa
maandishi, akithibitisha kauli yake kuwa ameahirisha ndoa na ameshaondoka Mbeya
kwenda Tunduma.
Kwa mujibu wa mpambe huyo, walikwenda kanisani na
kutokana na hali hiyo, Mchungaji Mwakijungu alilazimika kutangazia waumini hao
waliokuwa wakisubiri kushuhudia kiapo cha ndoa kwa vijana wao, kuwa ibada hiyo
imeahirishwa bila kutamka siku itakayofungwa.
Sherehe
Licha ya mkasa huo ambao ni nadra kutokea duniani
kuibua maswali mengi, ndugu wa upande wa mwanamume na wageni waalikwa ambao
katika harusi za siku hizi mialiko hutolewa kwa waliochanga, waliendelea na
sherehe iliyokuwa imeandaliwa.
Sherehe ya harusi ilipangwa kufanyika kwenye ukumbi
mmoja jijini Mbeya, ambapo ilipotimu saa mbili usiku, wageni waalikwa na ndugu
wa upande wa mwanamume waliwasili tayari kwa sherehe.
Mwandishi wa gazeti hili alifika ukumbini hapo, na
kabla ya kuanza kwa sherehe hizo, mshereheshaji alialika mwakilishi wa familia
ya upande wa Bwana harusi kueleza kilichojiri.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya ndugu wa Bwana
harusi, msemaji wa familia hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph,
aliwaomba radhi waalikwa na kuwataka wachukulie tukio hilo kuwa ni mapito tu.
“Mkiwa wazazi hakuna jambo jema kama kumpa zawadi
mtoto wenu halafu akawashukuru,” alisema mwakilishi huyo bila kutoa ufafanuzi
wa zawadi na shukrani na akaendelea:
“Naomba radhi sana kwa yaliyotokea, naomba tuzidi
kuwaombea vijana wetu kuhusu shetani aliyeamua kujinyanyua juu yao,” alisema
Joseph kwa niaba ya familia ya Mwakalobo.
0 comments:
Post a Comment